Tripoli, Libya
Ndege binafsi ya Aliyekuwa Rais wa zamani Nchini Libya, Hayati Muammar Gaddafi imepokelewa jana usiku Juni 22, 2021 katika mji mkuu wa Libya Tripoli baada ya karibu Miaka 10 ikiwa Nchini Ufarasa.
Ndege hiyo aina ya Airbus A340, iliyopokelwa na Waziri Mkuu wa Libya, Abdul Hamid Dbeibah, ambaye alikuwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa.
Pia kupitia Ukurasa wa Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Waziri Dbeibah ameandika kuwa ukarabati wa ndege hiyo na taratibu nyingine vimekamilika, na serikali ya mpito imelipia gharama zilizohitajika kuirejesha Libya.
Waziri Dbeibah ameongezea na kusema ndege nyingine 14 aina ya jet zilizosalia, 12 kati yake zimepangiwa kurejea Libya, huku serikali ikishughulikia kurejea kwa ndege mbili bora zaidi.
Taarifa iliyotolewa na Kituo cha televisheni ya Al Arabiya, kimesema kuwa jet ya Gaddafi, ambayo inafahamika kama “Kasri inayopaa”, ilipaa kimo cha chini juu ya mji wa Tripoli na kuyazunguka maeneo kabla ya kutua ardhini.
Waziri Dbeibah alizungumza na waandishi wa Habari amesema ndege hiyo watu wa Libya ndio watakaoamua hatma yake na kama itatumiwa na maafisa au watu wengine.
Rais Gaddafi ambaye aliiongoza Libya kwa muda wa miongo sita na ambaye anafahamika kama kiongozi aliyekuwa na nguvu za mamlaka kibinafsi ambaye alionekana katika jukwaa la dunia kama mwenye mtindo wake wa uongozi, aliuawa katika mji wa nyumbani kwa Sirte mwezi Oktoba 2011 wakati wa mzozo ulioibuka kufuatia uasi mwezi Aprili mwaka huo.
Serikali ya Umoja wa kitaifa (GNU) inayoongozwa na Dbeibah, iliingia madarakani baada ya kuchukua mamlaka kutoka kwa serikali iliyokuwa na makao yake mjini Tripoli na iliapishwa mwezi Machi kufuatia uchaguzi uliofanyika mapema mwaka huu katika mchakato uliodhaminiwa na Umaoja wa Mataifa.