Na Koku David, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa kupata Elimu ya Kodi ni haki ya Mfanyabiashara na kwamba itaendelea kuwaelimisha mara kwa mara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Juni 17, n2021 wakati wa kampeni endelevu ya Elimu ya Kodi ya Mlà ngo kwa Mlango inayoendelea nchini, Afisa Mwandamizi Mkuu wa Kodi wa TRA, James Ntalika amesema kuwa sambamba na haki pia mfanybiashara ana wajibu wa kulipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.
Amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kila mfanyabishara anapata elimu ya kodi ikiwa ni pamoja na kutambua haki na wajibu wake kama mfanyabishara.
“Pamoja na kupata elimu ya kodi, pia mfanyabishara ana haki ya kupinga makadirio ya kodi atakayokuwa amekadiriwa iwapo atahisi si sahihi lakini pia ana haki ya kusikilizwa iwapo atakuwa na kero na kutatuliwa kero hizo.
“Kwa upande wa wajibu, mfanyabishara pia anawajibu wa kutunza kumbukumbu ili kuepuka malalamiko ya kukadiriwa kodi ambayo si sahihi lakini pia kushirikiana na maofisa wa TRA,” amesema Ntalika.
Naye, Siriwa Chama ambaye ni Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, amesema kuwa katika kampeni hiyo, wafanyabiashara wengi wameonyesha uelewa wa umuhimu wa kodi isipokuwa wanahitaji kupewa elimu ya mara kwa mara ili kuwawezesha kuwa na utayari wa kuilipa kwa hiyari.
Amesema kampeni hiyo ni endelevu na kwamba TRA imejipanga kuhakikisha inamfikia kila mfanyabishara.
Fahim Ally ambaye ni mfanyabishara wa duka la vifaa vya umeme katika maeneo ya Msasani jijini hapa amesema TRA inafanya vizuri kuwapitia wafanyabiashara katika maeneo yao biashara ili kuwapa elimu ya Kodi na kwamba inawapunguzia usumbufu wa kwenda kupanga foleni katika ofisi za TRA ambako kunapoteza muda.
Anasema pia kupata baadhi ya huduma kwa njia ya mtandao kumerahisisha ikiwa ni pamoja na kuokoa muda.
Anasema ili kuwawezesha kulipa kodi kwa hiyari, ameitaka TRA kujikita zaidi kwenye elimu badala ya kusubiri wakosee na kuwatoza faini.
Naye, Mbuko Mhella mfanyabishara wa duka la nguo anasema TRA ya sasa imekuwa na uvumilivu kwa wafanyabiashara ambao hushindwa kulipa kodi kwa wakati kutokana na ugumu wa biashara uliopo.