27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Ujumbe wa Wanafunzi wawatoa machozi viongozi

Na Allan Vicent, Kaliua

Ujumbe wa kupinga vitendo vya kubakwa na kutumikishwa katika kilimo cha tumbaku na kazi nyingine ngumu uliotolewa jana na watoto wa shule za msingi wilayani Kaliua mkoani Tabora umesisimua viongozi, wazazi na walezi na kusababisha watokwe na machozi.

Wakiwasilisha ujumbe huo kwa masikitiko kwa njia ya ngonjera katika maadhimisho ya siku ya kupinga utumikishwaji watoto yaliyofanyika leo Jumatano Juni 16, 2021 katika kijiji cha Mtakuja kata ya Igagala wilayani humo walisababisha viongozi, wazazi na walezi kushikwa na simanzi kubwa baada ya kuguswa na ujumbe huo.

Mtoto wa Darasa la 3 katika shule ya msingi Igagala no.5, Sandra Yusuph (10) alisema dunia imejaa magonjwa mengi, watoto wanatumikishwa na wengine kubakwa bila hata aibu na kuhoji maadili ya jamii kwa watoto yako wapi.

Sandra aliendelea kubainisha kuwa mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, wewe unayemtesa unaharibu zawadi yako mwenyewe, mpe malezi bora mtoto wako ili akufae siku zijazo na uzeeni.

Nae, Mtoto Matilda Gaspar (11) wa Darasa la 4 katika shule hiyo alisema wale wote wanaowafanyia vitendo viovu watoto Mungu anawaona na hukumu itawakuta, mlezi wa watoto ni Maulana hivyo ukimtesa mtoto hutabaki salama.

Shakira Salimu (11) wa Darasa la 4 katika shule ya msingi Igagala no.6 alisema utumikishwaji mtoto ni dhambi isiyo kifani iwe kwa mzazi au mlezi, anapaswa kupakatwa miguuni, kupigiwa zeze na kupewa haki yake na sio kumdhalilisha.

“Mtoto ndiye taifa la kesho na mlezi wa wazazi wake, kama ataendelea kudhalilishwa, kutumikishwa au kubakwa, ni nani atakayekulea wewe mzazi na taifa litaongozwa na nani,” alihoji kwenye ubeti wa ngonjera.  

Oliva Norbet (10) wa Darasa la 3 katika shule ya msingi Kakobe alisema mwanga bora kwa mtoto ni elimu, siyo kumpa kazi ngumu zitakazomuumiza na kumzuia kwenda shule, utumikishwaji watoto unaua ndoto zao.

Upande wake, Helena Andreaa ambaye ni Mzazi na mkulima mkazi wa kijiji cha Igagala alitoa wito kwa wazazi kubadilika na kuacha kuwatumikisha bali wawapeleke shule ili wakasome.

Mwalimu Yusuph Ramadhani wa shule ya msingi Igagala alisema watoto wanapata taabu sana wakati wa kilimo, wanawalazimisha kwenda kupalilia mashamba ya tumbaku badala ya kuwaacha wasome.  

Godwin Gwasa, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Igagala aliwataka wazazi kutojihusisha na vitendo vya kutumikisha watoto wao katika kazi za kilimo, na kuitaka serikali kutoa adhabu kali kwa wale wote ambao hawataki kubadilika.

Upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Abel Busalama akiongozana na viongozi na wageni waalikwa waliwazawadia fedha taslimu zaidi ya Sh 50,000 na kuwapongeza kwa ujumbe mzuri ambao uligusa kila mtu na kusababisha watokwe na machozi.

Aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mzazi au mlezi yeyote atakayebainika kumzuia mtoto wake kwenda shule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles