Na Upendo Mosha, Moshi
Mkuu mpya wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai amewaonya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kutimiza wajibu wao kikamilifu na kutatua migogoro na changamoto zinazowakabili wananchi.
Kagaigai alitoa agizo hilo,jana wakati wa zoezi la kukabidhiwa ofisi na Mkuu wa mkoa mstaafu, Anna Mgwhira, Mjini Moshi ambapo amesema baadhi ya watendaji na viongozi wa serikali wamekuwa wakishindwa kutatua matatizo ya wananchi na serikali kuonekana haifanyi kazi jambo ambalo si sahihi.
Amesema ni wajibu wa wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri pamoja na watendaji kutimiza wajibu wao kwa weledi,uadilifu na uaminifu kwa maslahi mapata ya nchi badala ya kugeuka kuwa kero kwa wananchi.
“Nitoe agizo kwa wakuu wa wilaya,wakurugenzi na watendaji mkanisaidie kutatua changamoto za wananchi na malalamiko na kero zao maana sitakubali mimi kuwajibiswa kutokana na utendaji mbovu usioridhisha,”amesema Kagaigai.
Aidha, amesema malalamiko mengi yamekuwa yakienda ngazi za juu kutokana na kuwepo kwa uzembe wa utatuzi wa changamoto hizo kwa ngazi za chini na kwamba yeye hatokubali hali hiyo bali atafanya siasa na utendaji kwa maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mastaafu, Anna Mgwhira amesema jitihada mbalimbali zinahitajika katika kuhakikisha miradi ya maendeleo aliyoiacha inaendelea kwa maslahi ya uchumi wa wananchi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amewataka Wakuu wa Idara pamoja na maafisa Kilimo kuacha kukaa maofisini badala yake kutoka na kwenda kutatua matatizo ya wananchi ikiwemo wakulima.