KOCHA Mkuu wa timu ya Mwadui FC ya Shinyanga, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’,
amewatupia lawama waamuzi wanaochezesha michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akidai kuwa wanashindwa kutafsiri sheria 17 za soka.
Julio alitoa kauli hiyo juzi, mara baada ya kumalizika kwa pambano lao la Ligi Kuu dhidi ya African Sports, lililopigwa katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ambapo timu yake ilichapwa bao 1-0.
Julio alisema waamuzi wanaopindisha sheria zinazosimamia soka, wamekuwa chanzo kikubwa cha kudidimiza soka la Tanzania, kwani wanachangia sana kushuka kwa kiwango badala ya kupanda kama zilivyo nchi nyingine barani Afrika.
“Mimi nadhani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi wanatakiwa kusimamia kwa umakini michuano ya Ligi Kuu kwa lengo la kuongeza ushindani na ladha ya mashindano kama ilivyokuwa msimu
uliopita,” alisema Julio.
Pamoja na kocha huyo kulia na waamuzi, lakini wachezaji wa timu hiyo walishindwa kuonyesha umahiri na kiwango cha juu katika mchezo wa juzi kwa kushindwa kuzitumia vyema nafasi walizopata.
Naye kocha mkuu wa African Sports, Aluko Ramadhani, alisema hawana budi kushukuru kupata pointi tatu muhimu ambazo zimewapa
nguvu ya kufanya vizuri kwenye mechi zinazofuata Ligi Kuu ili kujinusuru kushuka daraja.