27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yarekebisha kipengele cha ukusanyaji mapato

2Elias Msuya, Dodoma

SERIKALI imebadilisha kipengele cha mwongozo wa Mpango wa Kuandaa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 unaotaka mapato yote yakusanywe na Wizara ya Fedha na Mipango.

Badala yake imesema baadhi ya taasisi za serikali zikiwamo mamlaka za serikali za mitaa zitaendelea kutumia utaratibu wa zamani wa kukusanya na kupanga bajeti kulingana na makusanyo yao.

Akizungumzia utaratibu huo,Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepewa madaraka hivyo ni lazima zikae na fedha zinazokusanya.

“Serikali za Mitaa zinaendesha huduma za jamii kama afya na elimu, ni lazima ziwe na fedha. Fedha hizo ndizo tunazipeleka kwenye huduma,” alisema Simbachawene.

Alisema hata utoaji wa elimu bure unategemea fedha hizo na haupaswi kufanyiwa siasa.

“Elimu ya bure isifanyiwe siasa, tunawapa walimu kubuni michango. Lakini sasa tunatoa Sh540 kwa mwanafunzi kwa mwezi, kwa kuwa mwaka haujaisha na wanafunzi wa sekondari Sh3600 kwa mwezi,” alisema Simbachawene.

Alisema tofauti na Serikali za Mitaa, yapo mashirika ambayo hukusanya fedha nyingi lakini hayana huduma wanazolazimika kutoa kwa wananchi hivyo yanatakiwa kubanwa kuliko kuondoa fedha Serikali za Mitaa.

Awali akisoma hotuba ya mwongozo huo wa bajeti bungeni jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alisema mapato yote yatakusanywa na Wizara ya Fedha na Mipango.

“Hivyo basi, maofisa masuuli wa wizara za Serikali, wakala, taasisi, Sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa watatakiwa kuwasilisha mapato yote yakayokusanywa kwenye mfuko mkuu wa Serikali na yatagawiwa kulingana na bajeti za mafungu zitakazoidhinishwa,” alisema Dk. Mpango.

Vilevile Waziri Mpango alisema utaratibu wa ‘retention’ uliokuwa ukitumika awali umefutwa na badala yake mapato yote yatakusanywa na kuwasilishwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali na kila fungu litapewa fedha kulingana na bajeti yake.

Hoja hiyo ililalamikiwa na baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliyeitaka Serikali kufikiria vyanzo zaidi vya mapato kwa halmashauri.

Wabunge wengine waliopinga kipengele hicho ni   Riziki Ngwali (CUF) kutoka Mafia, na Mbunge wa Babati Mjini Pauline Gekul akisema utaratibu huo ulishafanywa na Mwalimu  Nyerere miaka ya 1980 na ulishindwa.

Katika hatua nyingine, suala hilo limefika kwenye vikao vya ndani vya CCM huku wabunge wa chama hicho wakitaka hoja hiyo iondolewe.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles