26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji ya vikongwe yamebaki historia- RC Shinyanga

Na Anthony Ishengoma,Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amesema Mkoa wa Shinyanga hauna tena mauaji ya vikongwe kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na vyombo vya vya ulinzi na usalama zilizofanikisha kuyakamata makundi ya mapanga yaliyokuwa yanatekeleza mauaji hayo mkoani Shinyanga.

 Baadhi ya washiriki wa kikao cha Championi wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja jana mara baada ya kushiriki kikao hicho.

Telack alisema hayo wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha siku moja na Shirika la Msichana Initiative na Championi wa kutokomeza ndoa za utotoni mkoani Shinyanga kilichowakutanisha baadhi ya wabunge ambao wanaunda kikundi hicho pamoja na wadau wengine waliokutana leo kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Telack aliongeza kuwa kipindi cha nyuma vyombo vya habari kila kukicha vilikuwa vinaandika sana kuhusu mauaji ya mama wazee waliokuwa wanauawa kutokana na ramli chonganishi lakini sasa hali ni shwari na vyombo vya habari havitoi tena habari za mauaji hayo kwani hayapo tena.

Kuhusu mimba na ndoa za utotoni, Telack alisema kuwa juhudi zilizofanyika ni pamoja na kukamata watoto wakiwa wanafungisha ndoa na juhudi hizo zilifanyika baada ya Mkoa huo kuwa na takwimu za juu kwani awali Mkoa wa Shinyanga uliongoza kwa asiliamia 59 ya ndoa za utotoni nchini.

Telack alisema msukumo wa mikakati ya kupambana na mimba na ndoa za utotoni ulitokana na Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii kutoa takwimu hizo kwa Mkoa wa wake wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Mtoto wa Kike yaliyoadhimishwa Kitaifa Mkoani Shinyanga mwaka 2016. 

Telack aliongeza kuwa wanaume ambao wamekamatwa kwa kuwapa mimba watoto wa shule wamekuwa wakipata kifungo cha miaka 30 jela pomoja na changamoto ya baadhi ya Wazazi kushawisi watoto wao wasitoe ushahidi mahakamani lakini pia na wasimamizi wa sheria kwa kushirikishwa katika masuala haya kwa sasa hakuna ucheleweshaji kesi hizi.   

Telack amewataka wanaume kutambua kuwa mtoto wa mwenzeke mwenye umri sawa na mtoto wake sio mke kama ilivyo kwa mtoto wake hivyo wawachukulie watoto wa wenzao kama watoto wao na hivyo kukomesha vityendo vya mimba na ndoa za utotoni ili kutoa fursa kuwalinda watoto wakike.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amewaambia wabunge machampioni wa kutokomeza ndoa za utotoni kuwa lengo la kikao hiki ilikuwa ni kuwapa fursa kwao kufahamu juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Shinyanga katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili iwe fursa kwao kutumia uzoefu huo kwa bunge lakini pia katika maeneo yote ya Tanzania.

Aidha, Ng’washi Kamani, Mbunge Viti  maalum Vijana Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa anafahamu sana mira na desturi za wasukuma na madhara yake kwa wanawake na hivyo kutumia fursa hiyo kupongeza juhudi za mkoa na kuwataka wazazi mkoa wa Shinyanga kuwasomesha watoto wakike ili waweze kufikia ndoto zao.

Ng’washi amewataka wazazi kote nchini kujifunza kutokana na uwepo wa mwanamke mwenye nafasi ya juu ya uongozi Nchini akimtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwanamke na hivyo kuwataka kusomesha watoto wakike wakiamini kuwa ipo siku mtoto wao anaweza kubahatika kushika kiti kikubwa cha uongozi.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Wanawake Waislam na Mbunge wa Zamani wa Bungela la Jamhuri wa Tanzania, Shamim Khani amewataka wabunge ambao ni Chamipioni wa Ukatili wa Ndoa za Utotoni kukaribisha Uongozi wa Mkoa Bungeni kwa lengo la kutoa Elimu hii kwa wabunge ikiwemo pia kutambulisha Mkakati wa Mkoa wa Kukambana na Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto. 

Shamimu amewataka viongozi wa dini hapa Nchini kutumia nafasi waliyonayo katika jamii kutoa elimu kwa wafuasi wao kuhusu utokomezaji wa mimba na ndoa za utotoni kwa kuwa wanayo nafasi kubwa zaidi ya kushawishi jamii kutokomeza vitendo hivyo.

Naye Championi wa Ukatili dhidi ya Wanawake na watoto Mbunge, Aidha Kenani amesema kuwa ili kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake hatuwezi kumuacha mdau muhimu mwanaume kwani wanawake peke yake hawataweza bila kuanza na chanzo cha ukatili.

Kenani Aliongeza kuwa wabunge wako hapa kujifunza mbinu zilizotumiwa na mkoa wa Shinyanga kukomesha ukatili inabidi kuigwa ili ziweze kutumika maeneo mengine kwa kuwa tatizo hili haliko Shinyanga peke yake bali ni Tanzania nzima uku akiwaimiza viongozi wa dini kuimiza waumini hao kuacha dhambi ya uzinzi.

Mkoa wa Shinyanga tayari umekamilisha na kuzindua Mkakati wa Kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkakati unaotokana na Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ujalikanao kama NPA-VAWC 2017/18-2021/22.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles