WAZIRI wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe jana alilazimika tena kutoa ufafanuzi wa ununuzi wa mabehewa 274 ya treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) yaliyonunuliwa wakati akiwa Waziri wa Uchukuzi baada ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kudai kuwa ni mabovu.
Juzi bungeni Waziri Mwakyembe alisimama na kutoa ufafanuzi wa mabehewa hayo huku akisema yuko tayari hata kujiuzulu ubunge kama kashfa hiyo ni ya kweli.
Katika mkutano wa jana ulioonekana kumwelemea Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, wabunge wengi walizozana wakitaka miongozo na utaratibu.
Akizungumza jana jioni, Mdee alisema katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2011/12-2015/16, Serikali ilipanga kukarabati reli ya kati kilometa 2700, lakini hadi sasa zimekarabatiwa kilometa 150 tu.
“Mabehewa 274 ya Mwakyembe tumeambiwa na wenyewe ni feki, Sitta (Samuel) katuambia, akaunda ka kamati kake pale,” alisema Mdee na kukatishwa na sauti ya Waziri Mwakyembe akitaka kutoa taarifa.
“Naomba niende kwenye ile kanuni ya 63 (3) ili nimweleze … nataka nimweleze, mwanafunzi wangu na mbunge wangu wa Kawe… hapa ni bungeni hakuna ubabe. Leo nikimwambia Halima aniletee mabehewa ambayo hayafanyi kazi, atashindwa kunionyesha,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza:
“Wewe ni msomi wa sheria, kwenye mikataba kuna kipengele kinaitwa ‘defect liability period’… alisema huku akikatishwa na wabunge wa upinzani waliotaka kutoa taarifa.
Wakati huo alisimama Mdee akimtaka Dk. Mwakyembe aseme kama amevunja kanuni gani ili aijibu.
Lakini Dk. Mwakyembe akajibu: “Tuko kwenye kikao au ni vurugu kama Kariakoo?…Halima sikiliza, kama ni ubabe kaufanye huko nje…” alisema Dk. Mwakyembe huku akisoma kanuni ya 63(3 na 4).
Alipomaliza ndipo Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu wa Bunge, Ajira na Vijana, Jenister Mhagama aliposimama na kutoa utaratibu.
“Mwenyekiti kuhusu utaratibu Kanuni ya 68(8) naomba mwongozo wako, Bunge hili linaongozwa kwa kanuni, akishasimama mtu kuzungumza mwingine anasubiri mpaka mwenzake amalize kuzungumza. Hivi kwa nini watu wanavunja kanuni tu, vurugu tu halafu hawachukuliwi hatua?” alihoji Mhagama.
Mwenyekiti alisema bunge linaendeshwa kwa kanuni na sheria huku akiwataka watoa taarifa kufuata utaratibu.
Baada ya mvutano huo, Waziri Mwakyembe aliendelea:
“Msomi huyu anasema kuna mabehewa 274 feki, it is a lie (ni uongo), nikimwambia anionyeshe hawezi.
“Mabehewa yote yanafanya kazi kwa sababu yalipoletwa ni mimi mwenyewe niliyesema kuna mabehewa ambayo siyo mazuri, nikaunda uchunguzi, kwa sababu tulikuwa na haki chini ya mkataba ‘defects liability period’ ilikuwa ndani ya mwaka mmoja, wakaja wale waliotuuzia mabehewa wakayatengeneza, sasa yako wapi hayo mabovu,” alisema Mwakyembe.
“Hatuwezi kusikiliza watu ambao hawana hoja ya msingi. Suala hili tulishalitolea mwongozo juzi, Halima anakuja na porojo hapa,” aliongeza Dk. Mwakyembe.
Baada ya ufafanuzi huo, Mdee alisema taarifa yake ilitokana na taarifa ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi baada ya Dk. Mwakyembe ambaye alisema kuna mabehewa feki.
Kuhusu barabara, Mdee alijikuta katika mzozo mwingine baada ya kutaja jina la Rais John Magufuli.
Hapo Naibu Waziri wa Afya, Dk. Khamis Kigwangala alisimama na kutaja kanuni ya 64(1d) akisema:
“Mbunge yeyote hatatumia vibaya jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi bunge kuamua jambo lolote kwa namna fulani”.