NA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM
KOCHA Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema ushindani wa namba kwa wachezaji ndani ya kikosi hicho umechangia kupanda kwa kiwango cha timu hiyo kutokana na kila mmoja kupigania nafasi yake.
Juzi Simba waliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya African Sports ya Tanga, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambao uliwawezesha kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tangu kocha huyo raia wa Uganda apewe majukumu ya kukinoa kikosi hicho, ameonyesha mafanikio makubwa baada ya kushinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Mtibwa Sugar, JKT Ruvu na African Sports.
Akizungumza mara baada ya mchezo wa juzi, Mayanja aliwapongeza wachezaji wake kwa kuzidi kuimarisha viwango vyao na kufuata kwa umakini maelekezo anayowapa.
“Kadiri siku zinavyokwenda wachezaji wanazidi kuimarika na kuzidi kuzitendea haki nafasi wanazocheza ili kuiletea timu mafanikio na kujisogeza nafasi za juu zaidi katika msimamo wa ligi,” alisema.
Alisema pamoja na kufanikiwa kupata ushindi dhidi ya African Sports, bado wapinzani wao ni wakali na wamesajili wachezaji wazuri waliokuwa wakijaribu kuwafunga lakini hawakubahatika kufikia malengo yao.
Mganda huyo alisema kwa sasa wanaelekeza nguvu katika mchezo unaofuata dhidi ya Mgambo Shooting, ambao unatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Kutokana na ushindi wa juzi, Simba imeendelea kutetea nafasi yake ya tatu ikiwa imejikusanyia pointi 36 baada ya kushuka dimbani mara 16.