NA OSCAR ASSENGA, TANGA
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema makosa mawili yaliyofanywa na wachezaji wake kipindi cha pili ndio yaliwagharimu na kusababisha kupata kipigo cha kwanza ugenini dhidi ya Coastal Union.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, juzi walianza vibaya mzunguko wa pili wa ligi baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Pluijm alisema kipindi cha kwanza
walicheza vizuri lakini makosa ya kizembe yalichangia kufungwa bao kabla ya kwenda mapumziko.
Alisema wachezaji walirudi uwanjani kipindi cha pili wakiwa na ari kubwa ya kutaka kusawazisha bao hilo na hatimaye kuibuka na ushindi, lakini kasi yao haikuweza kuzaa matunda na kujikuta wakiambulia kipigo kutoka kwa wapinzani wao.
“Makosa haya yamechangiwa na wachezaji kutojitambua uwanjani kwa kushindwa kuonyesha nia ya kupata bao baada ya wapinzani kuanza kutumia mbinu za kucheza pasi ndefu tofauti na uchezaji wao,” alisema.
Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema mchezo umemalizika na wamefungwa lakini wanarudi kujipanga upya ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi inayofuata, kwani kikosi chake kina uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi ya wapinzani wao.
Wakati pambano la Yanga na Coastal Union likiendelea, katika hali isiyotarajiwa mashabiki wa timu hizo ambao walikuwa wakirushiana maneno makali na vijembe, walianza kuzichapa uwanjani baada ya ‘Wagosi’ hao kupata bao la kwanza.
Vitendo vya kurushiana maneno ya kuudhiana viliendelea hadi kipindi cha pili, ambapo Coastal Union waliandika bao la pili na kuzidi kuwachanganya mashabiki wa Yanga ambao walilazimika kuhama kwenye jukwaa lao na kuhamia kwa wapinzani wao lakini polisi waliwarudisha.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa kitendo kilichofanywa na makomandoo wa Yanga cha kuwafukuza mashabiki wa mkoani hapa wasishuhudie mazoezi ya timu hiyo kabla ya mchezo wa juzi, kinatajwa kuwa ni moja ya sababu iliyochangia kipigo hicho.
Inadaiwa kuwa makomandoo hao waliamua kuwatimua mashabiki kutokana na kuhofia kuhujumiwa, jambo ambalo lilipingwa vikali huku wakidai kuwa kitendo hicho kimeonyesha wazi kuwa wamedharauliwa.