Na TUNU NASSOR,DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ameshauri kuanza matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundisha ngazi zote za elimu ili kuwasaidia wanafunzi kufaulu kwa sababu ndiyo wanayoilewa vizuri.
Akizungumza wakati kukabidhi zawadi za mashindano ya mashairi yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Mwinyi alisema inawezekana kabisa kupata wasomi waliofikia hatua kubwa kwa kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili.
‘Ifikie wakati sasa mwanafunzi anapoanza shule ya msingi hadi anamaliza chuo kikuu anatumia Kiswahili hata kufikia ngazi ya profesa na lugha nyingine zikafundishwa kama lugha tu,” alisema Mwinyi.
Aliwataka waandishi wa habari kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha kwa kuwa ndio wanaoifanya lugha hii kukua.
“Niwaombe waandishi wa habari, wahariri na magwiji katika tasnia kuendelea kukipigania Kiswahili kiweze kuzungumzwa kwa ufasaha zaidi,” alisema.
Alimpongeza Rais Dk.John Magufuli kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika mazungumzo yake yote rasmi.
Aliwataka Watanzania kutumia lugha ya Kiswahili katika mazungumzo yao ya kila siku na kukifanya kifike nje ya mipaka ya Tanzania.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita ambae alihudhuria hafla hiyo alisema wanafunzi wamekuwa wakichelewa kuelewa maarifa yanayotolewa kwa lugha ya kiingereza.
Alisema inawawia ugumu wanafunzi wanapoingia sekondari kujifunza lugha mpya huku walipokea maarifa.