28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONTENA YA MAKONDA YAMWIBUA PROFESA MWANDOSYA



Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

SAKATA la makontena 20 yaliyoko Bandari ya Dar es Salaam kwa jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limemwibua waziri wa zamani katika Serikali ya awamu ya nne, Profesa Mark Mwandosya akikumbushia misingi ya utawala bora.

Makontena hayo yaliyokwama bandarini baada ya Makonda kushindwa kulipa kodi ya Sh bilioni 1.2, kwa mara ya pili juzi yalishindwa kuuzwa kwa mnada baada ya wanunuaji kushindwa kufikia bei.

Juzi, Profesa Mwandosya aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, akisema alivyofundishwa misingi ya utawala bora, mkuu wa nchi akimkosoa mtumishi hadharani, anapaswa kuandika barua ya kujiuzulu.

Ingawa hakumtaja Makonda moja moja, lakini ni wazi kuwa alimlenga mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuwa ni siku chache tu baada ya Rais Magufuli kumkosoa Makonda hadharani na kumtaka alipe kodi hiyo.

“Nilifundishwa misingi ya utawala, mkuu wa nchi akimkosoa mtumishi hadharani, unapeleka barua ya kujiuzulu ili kulinda heshima yake na kwa kufanya hivyo unajijengea heshima mbele ya umma. Nikiri kwamba huenda misingi hiyo imepitwa na wakati,”aliandika Profesa Mwandosya.

Alipoulizwa na gazeti hili kupitia simu yake ya  kiganjani, endapo ujumbe huo ulimlenga Makonda, Profesa Mwandosya alisema hakuandika jina la mtu bali anaelezea misingi ya utawala bora.

Gazeti hili lilipomwuliza ni kwanini aandike ujumbe huo wakati huu, alisema kwa ufupi: “Ujumbe unaweka wakati wowote na hili nililoandika ni somo katika utawala bora…andika hivyo hivyo kwenye gazeti lako,”.

Alhamisi ya wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli aliingilia kati mzozo kuhusu makontena hayo ambao ulianza tangu Machi mwaka huu, akimtaka Makonda alipe kodi.

Akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita, aliwataka viongozi wote kujenga utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa masilahi ya watu binafsi.

“Ni lazima sisi viongozi no matter uko kwenye position gani, tujenge mazingira ya kuwatumikia watanzania hizo ndizo sadaka zetu.

“Mmesikia hili sakata la Dar es Salaam eti Mkuu wa Mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi kwanini asilipe? Kwa sababu katika sheria za nchi yetu kwa mfano ni mtu mmoja tu aliyepewa dhamana kwa mujibu wa sheria ambapo ni sheria ya fedha, sheria ya madeni,  sheria ya dhamana na misaada.

“Nafikiri kupitia sheria namba 30 ya mwaka 1974 kifungu cha 3,6,13 na 15, ndiye amepewa dhamana ya kupokea misaada kwa ajili ya nchi hakuna mtu mwingine hayupo.

“Sasa ukichukua makontena kule umezungumza na watu wengine au na wafanyabiashara, unasema una makontena yako halafu unasema ya walimu wala hata shule hazitajwi.

“Hii maana yake nini? Si unataka utumie walimu ulete haya makontena utapeleka shule mbili, tatu, ndizo zitapewa mengine utakwenda kuyauza kwenye shopping mall lakini walimu walikwambia wanahitaji makochi! wafanyakazi wasitumike kwa masilahi ya watu fulani,”alisema Rais Magufuli.

Jumapili ya Agosti 26 mwaka huu, Makonda alifanya ibada maalumu ya kumwomba Mungu ili wanaofanya mnada wasipate wateja.

“Amelaaniwa mtu yule atakayenunua furniture (samani) za walimu. Nimefanya ibada maalumu ya kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa sababu naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wanaofanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni jitihada zangu binafsi.

“Leo TRA wameamua kuuza samani za walimu kwa wamiliki wa kumbi za starehe ili walimu waendelee kugombania madawati na vyoo na wanafunzi. Mimi Paul Makonda nimefanya kwa sehemu yangu, kilichobaki ni mwenye wazo atasimama siku moja kujitetea,” alisema Makonda.

Kauli hiyo ya Makonda ilimwibua Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango siku moja baadaye, aliyeapa kusimamia sheria na kuhakikisha makontena hayo yanapigwa mnada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles