Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WAGONJWA 56 wenye matatizo ya figo wanasubiri huduma ya upandikizaji figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imebainika.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Muhimbili, Onesmo Kissanga alisema hayo jana wakati alipokuwa akiwasilisha mada kwenye Kongamano la kwanza la sayansi hospitalini hapo.
Alikuwa akielezea kuhusu huduma za matibabu ya figo zinazotolewa hospitalini hapo hasa huduma mpya ya upandikizaji figo ambayo imezinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
“Magonjwa ya figo yapo katika kundi la magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ambayo takwimu zinaonyesha yanazidi kuongezeka, katika kitengo chetu tunahudumia wagonjwa wapatao 200 wenye magonjwa ya figo wanaopatiwa huduma ya kuchuja damu (dialysis) kwenye kitengo chetu,” alisema Dk. Kissanga.
Dk. Kisasnga alisema asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa hao wanahitaji huduma ya kupandikiza figo ambayo ni bora zaidi kuliko ile ya kuchuja damu katika kukabiliana na ugonjwa huo.
“Tumefanikiwa kumfanyia upandikizaji mgonjwa mmoja na hali yake inaendelea vizuri kama mnavyomuona (akionesha picha) hivyo hadi sasa tuna wagonjwa 56 wanaosubiri kufanyiwa upasuaji huo,” alisema Dk. Kissanga
Akizungumza na baadhi ya wagonjwa alipowatembelea katika chumba cha ‘dialysis’ Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile aliwahisi kuwa na subira wakati wakisubiri kufanyiwa upasuaji huo.
“Jambo la kwanza tulilofanya ni kujenga uwezo wa ndani, tumeongeza mashine za kuchujia damu kutoka 17 hadi 42 ili kusaidia wagonjwa wengi kupata huduma kwa wakati.
“Kumtibu mgonjwa mmoja nje ya nchi ni gharama kubwa mno, gharama tunazotumia nje ya nchi tuna uwezo wa kutibu watu wanne hadi watano ndani ya nchi.
“Serikali itaendelea kuboresha huduma za matibabu hapa MNH na katika hospitali nyingine zilizopo chini yake. Tunakusudia kuanzisha huduma hii hapo baadaye pia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma,” alisema Dk. Kissanga.