28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

SIYO KIKI… JOTI KUFUNGA NDOA LEO

Na CHRISTOPHER MSEKENA

MCHEKESHAJI maarufu kutoka Kundi la Orijino Komedi, Lucas Mhuvile ‘Joti’ leo anatarajia kuuaga ukapera kwa kufunga ndoa na mchumba wake wa siku nyingi anayejulikana kwa jina la Tumaini.

Joti ambaye staili yake ya kuigiza ni kuvaa uhusika wa rika zote, anafunga ndoa hiyo katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Magomeni, jijini Dar es Salaam ikifuatiwa na sherehe kubwa kwenye ukumbi wa Mlimani City.

Msanii huyo amethibitisha kuuaga ukapera baada ya wengi kufikiri huenda ni kiki au tangazo la biashara linalotarajiwa kutoka hivi karibuni.

Mwezi Februari mwaka huu mchekeshaji huyo aligonga vichwa vya habari za burudani baada ya kusambaa kwa video na picha zinazomwonyesha akiwa kwenye tukio la harusi lakini baadaye ikagundulika kuwa lilikuwa tangazo la kampuni moja ya mawasiliano nchini.

Tayari sherehe ya Send Off ya mke wake mtarajiwa imeshafanyika juzi Alhamsi na picha zinazomwonyesha Joti akiwa ukumbini kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Joti mwenyewe aliamua kuweka taarifa sahihi za ndoa yake hiyo kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akiambatanisha na picha yake akiwa ukumbini na bibi harusi mtarajiwa.

Joti aliandika: “Maraa paaah, walijua tangazo la TIGO kumbe kweli, nachukua jiko ukweni. Watu oyooooooooh.”

KIDUKU GUMZO

Katika sherehe hiyo iliyofanyika juzi Alhamisi jijini Dar es Salaam, Joti alizama ukumbini mbele ya wakwe zake kuchukua jiko akiwa na mtindo wa nywele unaofahamika kama kiduku jambo lililoibua gumzo kwani wengi walitarajia kumuona mchekeshaji huyo kwenye mwonekano tofauti na nadhifu kulingana na ukubwa wa tukio hilo.

Mashabiki wengi waliotoa maoni yao mitandaoni wameonekana kuchukizwa na mtindo wa kiduku alioibuka nao katika sherehe hiyo.

“Lakini ngoja tuone, ataingia hivyo hadi kanisani kweli au atanyoa?” aliandika mtoa maoni mmoja.

Hata hivyo, wengine walimpongeza kwa maelezo kwamba, kwa kazi yake ya sanaa suala la mitindo ni jambo la kawaida.

ASKOFU ATIA NENO

Katika upande mwingine Askofu William Mwamalanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili wa dini zote nchini, amepinga vikali mtindo huo wa nywele kwa maelezo kuwa hauna maadili.

“Huyo ni msanii na usanii ni sehemu ya kazi yake akiwa huko lakini anapokuja kwenye nyumba ya ibada, kanisa lina heshima na maadili yake na mtu anapoingia kanisani hawezi kuingia na kiduku.

“…na itakuwa ni aibu kwa mchungaji au kiongozi wa dini atakayefungisha ndoa mtu ambaye hayuko kwenye maadili, anaweza kunyoa nywele kimaadili kisha akimaliza anaweza kuendelea kuweka kiduku,” alisema Askofu huyo alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo katika redio moja jijini Dar es Salaam jana.

MASANJA AMPONGEZA

Joti anafuata nyayo za mchekeshaji na memba mwenzake wa Orijino Komedi, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ aliyefunga ndoa na Monica, miezi kadhaa iliyopita.

Msanii huyo ni miongoni mwa wengi waliotoa salamu za pongezi kwa Joti kwa kutumia kurasa zao katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Masanja aliandika: “Dogo (Joti) amefanya maamuzi ya kiume kwenda ukweni kuchukua mtoto wa watu. Unambadilisha jina la pili, mnaenda kanisani na ukumbini kisha geto na ndiyo inavyotakiwa kwa vijana wengine maana mambo ya kulala peke yako unajikunja kama korosho siyo poa. Joti amefanya uanamume.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles