CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi ametangaza kushuka kwa gharama za urasimishaji makazi kutoka Sh 250,000 inayotozwa hivi sasa na kampuni za upimaji na kuwa Sh150,000.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana katika kikao na wapimaji.
Alisema gharama zilizokuwa zinatozwa na kampuni za upimaji ni kubwa na kusababisha wananchi wengi kushindwa kumudu.
Alisema wenye makazi holela wengi wao wana vipato vya chini walishindwa kununua viwanja vya serikali vyenye hati hivyo kuwatoza gharama kubwa ni kuzidi kuwabebesha mzigo.
“Hakuna sababu za kutoza fedha nyingi kwani nimefanya utafiti na kubaini kampuni hizi zinajipatia fedha nyingi kwa kutoza Sh 250,000.
“Kwa hiyo kuanzia leo ninatangaza kushusha gharama hadi kufikia Sh 150,000 na kwa ambaye hawezi aache kazi hiyo,”alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi alisema hadi sasa kuna kampuni zaidi ya 70 ambazo zimesajiliwa upimaji lakini zinazofanya vizuri ni chache hivyo atahakikisha wanaofanya shughuli hiyo chini ya kiwango anawafutia vibali.
“Tumeshindwa kuchukua hatua kwa muda mrefu kuwafutia wapimaji wanaofanya kinyume kwa sababu mkurugenzi upimaji alikuwa hajateuliwa lakini siku si nyingi atateuliwa na hatua zitachukuliwa,” alisema Lukuvi.
Alisema urasimishaji ni haki ya kila mwananchi isipokuwa hauwahusu watu wanaoishi mabondeni kwenye ardhi oevu na maeneo ya huduma za jamii.
Hata hivyo alitoa onyo kwa wapimaji hao kuhakikisha wanasimamia shughuli za upimaji hadi mwisho na mmiliki wa ardhi abakie kulipa gharama tu.
Alisema zipo baadhi ya kampuni zimekuwa zikifanya kazi chini ya kiwango na kujivunia viongozi wa mitaa jambo ambalo si sahihi .
Aliagiza kuanzia sasa tenda za urasimishaji makazi zitolewa na halmashauri ya wilaya husika.
Pia alitoa onyo kwa watendaji wa wizara hiyo ambao wanamiliki kampuni za upimaji kuacha kutumia muda na vifaa vya ofisi kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
Lukuvi alisema pia kuwa shughuli za utoaji leseni za makazi zimeanza mkoani Dar es Salaam na hadi sasa watu 60,000 wamepata leseni hizo.
Alisema leseni hizo zinatolewa kwa gharama ya Sh 5,000 ambazo zinadumu kwa miaka mitano na zinatolewa kwa watu wasio na hati.
Alisema utoaji leseni utakuwa endelevu nchi nzima ambako kwa Dar es Salaam utafanyika kwa miezi mitatu na baadaye nchi nzima.
Alisema takwimu zilizopo zinaonyesha asilimia 70 ya wananchi hawalipi kodi hivyo shughuli za utoaji leseni zitasaidia ongezeko la mapato kwa kukusanya Sh bilioni 24.