26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Naibu Katibu Mkuu Chadema Mbaroni

RAYMOND MINJA-IRINGA

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) upande wa Zanzibar, Salumu Mwalimu, amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa.

Mbali na Mwalimu, wengine waliokamatwa ni Katibu wa Chadema wa mkoa huo, Jakson Mnyawami na Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Mbeya, Jailos Mwaijande.

Viongozi hao walikamatwa jana wakijiandaa kuingia kwenye kikao cha ndani wilayani Mufindi kwa lengo la kujadili uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Ilidaiwa kuwa hatua ya kukamatwa kwa viongozi hao ilitokana na agizo la Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William kwa kuwa ofisi yake haikuwa na taarifa ya kufanyika kwa kikao hicho.

Akizungumza na MTANZANIA, mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Suzan Mgonakulima, alisema wameshangazwa na kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Mufindi kutumia Jeshi la Polisi kuzuia mkutano wao wa ndani ambao uko kisheria.

Alisema walipofika kwenye ukumbi ambao walitarajia kufanyia mkutano huo, walikuta askari polisi wakiwa na silaha za moto wameuzunguka ili mtu yeyote asiweze kuingia.

“Tulikuta polisi wametanda kote na tulipowauliza kwanini wanatuzuia, wakasema wameagizwa na mkuu wa wilaya kuzuia mkutano wetu eti hatuna kibali.

“Tukawaambia huu mkutano hauhitaji kibali kwa kuwa ni mkutano wetu wa ndani wa chama, lakini hawakutaka kutusikiliza na mwisho wakatuambia tumtafute mwenyewe mkuu wa wilaya au OCD ili atupe ufafanuzi wa kina sababu za kuzuiwa mkutano wetu,” alisema Mgonakulima.

Alisema baada ya kauli hiyo ya polisi walianza mchakato wa kumtafuta mkuu wa wilaya na OCD, lakini simu zao zilikuwa zikiita kwa zaidi yasaa mbili bila kupokewa.

Mgonakulima alisema walipoona simu hazipokewi waliamua kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, ili kujua sababu za kuzuiwa mkutano wao, lakini aliwajibu hana taarifa.

Alisema wakati viongozi wa mkoa wakiendelea kutafuta mwafaka, walishangaa baadhi ya polisi wakilifuata gari la Mwalimu ambalo lilikuwa umbali wa hatua 25 na kumshusha huku wakimpiga virungu na kwenda kumwingiza kwenye gari lao.

Mgonakulima alisema baada ya majibu ya polisi, walimpigiasimu Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Richard Kasesela, ambaye naye aliwajibu kwamba hajui kama kuna mkutano wa ndani ulizuiwa.

“Lakini baadaye tulimpigia tena Kasesela akatuambia kuwa mkuu wa wilaya alipata taarifa kuwa sisi Chadema Mafinga tuna mgogoro hivyo ingetokea vurugu, ndiyo maana wakazuia. Sasa tumewaambia watuletee huyo aliyeenda kulalamika kuwa tuna mgogoro, lakini mpaka muda huu hatuna majibu,”alisema Mgonokulima.

CHADEMA YALAANI

Dakika chache baada ya tukio la kukamatwa kwa viongozi hao, Chadema kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, ilitoa taarifa na kulaani tukio hilo.

“Tukio la kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu Mwalimu lilitanguliwa na kitendo cha askari takriban saba kumfuata na kumtoa ndani yagari kwa nguvu bila kutoa maelezo yoyote ya sababu ya kufanya hivyo,”  ilieleza taarifa hiyo.

Makene alidai kwamba takriban polisi 40 waliokuwa kwenye magari matatu wakiwa na silaha za moto walifika Ukumbi wa Mamu ambako maandalizi ya kikao hicho cha ndani yalikuwa yanaendelea, wakisema kuwa wameagizwa kuzuia kikao hicho na Mkuu wa Wilaya.

Alisema viongozi wote waliokamatwa wanashikiliwa Kituo cha Polisi Mafinga.

“Tunalaani na kukemea vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mwalimu akiwa na viongozi wengine na kumtendea kama mhalifu.

“Mwendelezo huu wa vitendo vya askari wa jeshi hilo kuvunja sheria za nchi na kuwanyanyasa viongozi wa upinzani nchini haukubaliki na unazidi kuchochea hisia kali za uonevu katika jamii,” alisema Makene katika taarifa yake.

KAULI YA DC

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu kukamatwa kwa viongozi hao,Mkuu wa Wilaya Mufundi, William, alisema awali walipokea taarifa kuwa mkutano huo ni wa wilaya, lakini intelijensia yao ilibaini ni wa kitaifa.

“Mikutano yoyote inayofanyika katika wilaya ni lazima tupate taarifa ili tuweze kutoa ulinzi na wanaofanya wafanye kwa amani. Hakuna nchi inayoweza kuendeshwa bila kufuata misingi ya sheria.

“Kama kuna mtu anafanya mkutano au kikao katika wilaya husika ni lazima atoe taarifa kwa kuandika barua kwa mkuu wa wilaya ili awezekutoa ulinzi kwa kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika wilaya husika.

“Sababu kubwa ya kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu (SalumMwalimu), baada ya Jeshi la Polisi kuzuia, aliwatangazia watu kwamba mkutano wao utaendelea kama kawaida na hakuna wa kuwatisha kwa sababu nchi ni ya watu wote.

“Baada ya kutoa kauli hiyo ilibidi polisi limchukue akiwana viongozi wengine hadi kutuo cha polisi kwa ajili ya kuchukua maelezo ya kwanini wanafanya mkutano bila kibali,” alisema.

Alisema kuwa baada ya viongozi hao kumaliza mahojiano na polisi aliagiza waachiwe na kama watataka kuendelea na mkutano wao itabidi waandike barua ya kuomba.

“Endapo wataandika barua ya kuomba kuendelea na mkutano huo basi wataendelea kama kawaida, kwa kuwa kila mmoja ana haki ya kufanya mkutano ili mradi hawavunji sheria,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles