25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada wa vyama vya siasa unatoa changamoto kwa vyombo vya ulinzi nchini

NA MAGOIGA SN

KWA mujibu wa ibara ya 147 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeeleza bayana kuwa ni marufuku mtu yeyote, au chama cha siasa au kikundi chochote hawataruhusiwa kuanzisha kikundi cha kijeshi, mgambo au kikundi cha ulinzi isipokuwa serikali pekee.

Kwa bahati mbaya sana, katiba za vyama mbalimbali vya siasa kama vile Chadema na CUF zilisajiliwa huku zikiwa na vipengele vinavyoeleza kuwa chama kitaanzisha kikundi cha ulinzi kama vile Redbrigade cha chama cha Chadema na Blue Guard kwa chama cha CUF.

Chama cha Mapinduzi kinatumia kikundi cha ulinzi kijulikanacho kama Green Guard lakini tofauti na vyama vingine vya siasa ambavyo katiba zao zimetaja kuhusu vikundi vyao vya ulinzi, katiba ya chama cha mapinduzi haijataja kuhusu kikundi cha ulinzi wa Green Guard, kwahiyo nitakuwa sahihi nikisema kilianzishwa lakini nje ya katiba.

Hili ni kosa ambalo lilifanywa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa uzembe au kutojua, nasema ni kosa maana katiba ya Tanzania ilikwishajieleza wazi kuhusu hilo, sasa ilikuweje msajili aruhusu katiba ya vyama hivyo kusajiliwa ilihali moja ya vipengele vinasema chama kitaanzisha kikundi cha ulinzi kitakachofanya kazi kama zinazofanywa na majeshi ya serikali?

Kwakuwa tayari yametokea tutafakari namna ya kurekebisha hilo hususani kipindi hiki ambacho tunajadili muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.

Muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa umetoa fursa ya kurekebisha haya makosa, kifungu cha 8(e) kimepiga marufuku kwa vyama vya siasa au kiongozi yeyote kuanzisha kikundi cha kijeshi, mgambo au kikundi cha ulinzi chenye lengo la kufanya kazi au shughuli zinazofanana na ulinzi zinazofanywa na jeshi la polisi au vyombo vingine vya ulinzi vya serikali nchini.

Kifungu kidogo cha 8(E)(2) kimeainisha kuwa, chama cha siasa hakitatoa fedha za kuratibu vikundi vya aina hiyo au kuratibu mafunzo ya kijeshi au matumizi ya siraha na kadhalika.

Kifungu hiki kinaenda kufuta moja kwa moja vikundi vya ulinzi kama Green Guard (CCM), Redbrigade (Chadema)  na Blue Guard (CUF). Kifungu kidogo cha 8(E) (3) kinasema chama cha siasa kitakachokiuka kifungu hiki kitafutiwa usajili na viongozi waliojihusisha na kosa hilo wanaweza kufungwa kifungo kisichopungua miaka 5 au kisichozidi miaka 20 au vyote kwa pamoja.

Tangu awali nimesema bayana kuwa ukiacha kipengele cha 6 , muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ya 2018 ni mzuri sana hususani katika kipindi hiki ambacho nchi inahitaji vyama vya siasa imara kama taasisi, vyama vyenye viongozi wanaozingatia katiba ya vyama vyao pamoja na kuheshimu sheria mbalimbali za nchi, vyama vinavyoheshimu uwazi katika mapato na matumizi pamoja na uwajibikaji wa viongozi.

Lakini kubwa zaidi ni kutimia kwa ndoto ya kuwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa mwenye nguvu kisheria ktk kuhakikisha kuwa sheria inayovisimamia vyama hivi inafuatwa kikamilifu.

Moja ya faida kubwa ya kifungu hiki ni kuwa kitasaidia sana kudhibiti vyama vya siasa kuacha kujijengea vikundi vya kijeshi kwa mwavuli wa vikundi vya kiulinzi wa viongozi wa chama husika.

Pili vikundi hivi vimekuwa vikituhumiwa kuendesha mipango ya vurugu na uvunjifu wa amani hususani nyakati za uchaguzi na mikutano ya kisiasa, hivyo kuvifuta kunaweza kusaidia kuongeza utulivu nyakati za uchaguzi.

Tatu, vikundi hivi vikiachwa vikakua na kujiimarisha vinaweza kugeuka kuwa vikundi vya kiasi iwapo vitaachwa vikaanza kufadhiliwa na mataifa ya nje yenye nia mbaya na nchi yetu, kisha kuweza kuleta vurugu au kuhatarisha amani yetu.

Pamoja na kwamba kuna faida kubwa kuvifuta vikundi hivi vya kiulinzi vinavyomilikiwa na vyama vya siasa kinyume cha ibara ya 147 ya katiba ya nchi, bado uzoefu unaonyesha kuwa suala la ulinzi na usalama limeonekana kuwa ni changamoto kubwa sana nyakati za uchaguzi.

Hii inatokana na ukubwa wa nchi yetu kijiografia pamoja na idadi kubwa ya watu ukilinganisha na idadi ya polisi katika kuhakikisha kuwa kila eneo linapata ulinzi wa uhakika wakati wote, lakini kibaya zaidi ni baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kuvitumia vikundi hivi kutisha wapiga kura na kuwatisha wagombea na wafuasi wa vyama vingine.

Kama umewahi kushiriki kampeni za uchaguzi au hata kugombea uenyekiti wa kijiji, mtaa, udiwani au ubunge utakubaliana na mimi kuwa suala la ulinzi na usalama nyakati za uchaguzi ni changamoto kubwa sana.

Kuna nyakati mnawahitaji polisi lakini wanakuwa hawatoshi kujigawa, mwisho wa siku mgombea usipokuwa na kikundi imara cha ulinzi hali huwa tete sana hususani maeneo ambayo polisi hawatoshelezi mahitaji ya ulinzi na usalama wa mali za raia.

Japo kiujumla tumeshuhudia faida kiduchu na madhara makubwa ambayo yamesababishwa na hivi vikundi vya kiulinzi. Nadhani huu ni muda muafaka wa kuvifuta vikundi hivi ambavyo vinatumika vibaya na ambavyo vimeanzishwa kinyume na katiba ya nchi

Vikundi hivi vikifutwa kwa mujibu wa muswada huu, inatoa changamoto kwa wizara ya mambo ya ndani na vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga upya na kujizatiti kikamilifu katika kukabiliana na vurugu za kisiasa zinazozuka maeneo mbalimbali hususani nyakati za uchaguzi.

Jeshi la Polisi likiweza kujizatiti katika hilo hakuna haja ya vyama vya siasa kuwa na vikundi vya kiulinzi vinavyotumiwa na wanasiasa kuleta fujo na kusambaza hofu.

Je, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaweza kuhakikisha uwepo wa ulinzi sehemu zote za nchi kwa wakati mmoja hususani nyakati za uchaguzi hapa nchini?

Hilo ndilo jambo la msingi tunaloweza kuliweka katika mjadala baada ya kuvifuta vikundi hivi, kama umewahi kushiriki katika chaguzi mbalimbali nchini utaelewa namaanisha nini.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles