Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameitaka Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu nchini, iongeze kasi ya kupambana na biashara hiyo ili iweze kudhibitiwa kwa kuwa inaichafua nchi.
Waziri Lugola, ambaye leo anatarajia kufungua mkutano mkubwa wa mafunzo kwa watekelezaji wa sheria ya kuzuia biashara hiyo haramu mjini Zanzibar, alisema wakati akijiandaa kufungua mafunzo hayo, lakini wahusika waweke mikakati thabiti ya kuidhibiti biashara hiyo.
Mafunzo hayo ambayo ni ya siku tano, yatatolewa kwa wadau wanaotekeleza sheria ya kuzuia na kupambana na biashara hiyo, maofisa polisi, Uhamiaji, waendesha mashtaka,mahakimu,maofisa ustawi jamii na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO’s) yaliyopo mjini hapa.
Waziri Lugola, alisema mkutano huo ni muhimu kwa wadau hao kupata mafunzo ya kukabiliana na mapambano ya biashara hiyo haramu ambayo Wizara yake itaendelea kuidhibiti.
“Nimealikwa kufungua mkutano huo, baada ya mafunzo hayo ya kitaalamu ambayo nimeambiwa yatakuwa ya siku tano, naamini maofisa watakaopewa mafunzo hayo kutoka wizara yangu na maofisa wengine wa Serikali kutoka sehemu mbalimbali nchini na NGO’s za hapa Zanzibar, watakuwa wamepikwa na kuiva na hatimaye watatusaidia katika kutekeleza sheria ya kuzuia biashara hii haramu ya usafirishaji wa binadamu,” alisema Lugola.
Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti hiyo kutoka wizara hiyo, Separatus Fella, alisema zaidi ya washiriki 80 watapewa mafunzo hayo na ana matarajio makubwa elimu watakayopewa itazaa matunda.
Alisema washiriki watapewa mafunzo mbalimbali, ikiwamo kujua kutofautisha makosa ya biashara haramu ya usafirishaji binadamu na mengine, na namna ya kupeleleza na kuendesha mashtaka.