Na MWANDISHI WETU-DODOMA
UTITIRI wa kodi ambazo zinalipwa na wawekezaji nchini bado umeonekana kuwa changamoto kubwa kwao na hivyo kutoa ombi kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kuangalia namna ya kupunguza utitiri huo wa kodi hizo.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni jijini hapa na Mkurugenzi wa Ushirikiano na Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Cetewico Limited, Katrin Boehl alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara katika kiwanda hicho.
“Kwa upande wangu lazima niseme nimeona ushirikiano wa hali ya juu katika Serikali yangu Dodoma kwani nikiwa na tatizo lolote ninakwenda katika ofisi za Serikali yangu ya Dodoma, hivyo imeonesha uthamini wa kiwango kikubwa wa kazi tunazofanya,” alisema Katrin.
Alisema kampuni yao inapongeza juhudi za Serikali katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda nchini ili kufikia uchumi wa kati na wamedhamiria kuunga mkono kwa vitendo kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu lakini changamoto kubwa ambayo wanakabiliana nayo ni uwepo wa kodi nyingi.
“Nampongeza sana Rais Dk. Magufuli pamoja na Serikali yake kwani tunaona dhamira njema katika kuhakikisha Tanzania inakuwa ya viwanda.Kampuni yetu tumekuwa tukipata ushirikiano mkubwa kutoka Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
“Hata hivyo kilio chetu ni wingi wa kodi ambazo zinasababisha kutumia fedha nyingi kwenye uzalishaji na matokeo yake bidhaa zetu zinakuwa juu kiasi cha kushindwa kuhimili ushindani wa soko.
Kutokana na utitiri huo wa makodi ambapo alihesabu zipo zaidi ya 13 , ametoa ombi kwa Serikali kuhakikisha wanakaa na kuangalia kodi na ikiwezekana zipunguzwe ili kurahisisha mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania huku akionesha kufurahishwa na kasi ya uwekezaji wa viwanda unaondelea nchini.