31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Utoro shuleni Bukombe 50% • Kuendekeza ngono, machimbo ya dhahabu vyachangia

Mwajuma Mohamed, mkazi wa Ushirombo wilaya ya Bukombe (15) akiwa amempakata mtoto wake wa miezi 7.Pendo Sungu amepata ujauzito akiwa bado mwanafunziNa Mariam Mkumbaru, Bukombe
MATARAJIO ya wazazi wengi ni kuona watoto wanapoanza shule wanahitimu masomo yao kwa kufikia ngazi za juu za elimu. Hata hivyo, matarajio hayo hayafikiwi katika maeneo mengi hapa nchini kwani watoto wengi hushindwa kuhitimu kutokana na tatizo la utoro.
Tatizo la utoro shuleni ni changamoto kubwa katika sekta ya elimu nchini kwani shule nyingi katika maeneo mbalimbali zinakabiliwa na changamoto hiyo. Miongoni mwa wilaya ambazo tatizo hilo ni kubwa ni pamoja na Wilaya ya Bukombe.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Amani Mwenegoha, anasema kuwa utoro katika shule za sekondari kwa wilaya hiyo upo kwa kiwango kikubwa sana kwani takriban nusu ya wanafunzi wote wanaoanza shule mbalimbali wilayani humo huwa hawamalizi masomo yao kutokana na utoro.
Mwenegoha anasema kuwa utoro katika wilaya hii upo kwa asilimia 48 hadi 50 kwa sekondari wakati kwa shule za msingi ni 26%. “Baadhi ya sababu zinachochangia hali hiyo ni kuwapo kwa machimbo ya madini pamoja na baadhi ya wazazi kutokuwa na uelewa mpana juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto.”
Anasema kuwa baadhi ya wazazi hawapendi watoto wao waende shule, badala yake wanawatuma kuchunga ng’ombe au kufanya shughuli nyingine.
Mwenegoha anasema kuwa, kwa sasa ofisi yake ikishirikiana na ofisi ya Afisa Elimu wana kazi ya kuwasaka wanafunzi wote walioacha shule na kufanyakazi ya kuchunga na kuchimba dhahabu katika machimbo mbalimbali.
Aidha, anasema kuwa sio tu kuwasaka wanafunzi walitoroka shule, bali pia msako unawalenga hata wanaume waliotelekeza familia zao na kuzifanya zikose mwelekeo mzuri wa maisha.
Anasema kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi shuleni pamoja na kupunguza pia tatizo la mimba za utotoni kwani baadhi ya wanafunzi wa kike wanaotoroka shuleni huishia kupata mimba.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ushirombo, Dionizimu Ruchengura, anasema kuwa utoro wa wanafunzi wa kike umekithiri kwa kiwango kikubwa kwa sababu ya kuwepo na machimbo mbalimbali ya migodi, hali ambayo inasababisha wasichana kurubuniwa na wachimbaji hao.
“Kinachochangia utoro kwa watoto wa kike katika shule mbalimbali za wilaya hii ni wanaume wenye pesa za madini wanaozitumia pesa hizo kuwarubuni watoto wa kike na kusababisha waache shule,”alisema Mwalimu Ruchengura.
Anasema kuwa utoro mwingi hutokea kipindi wanafunzi wanaporudi majumbani kwao kwa mapumziko. “Wakiondoka kwenda nyumbani, watoto wengi wa kike hawafiki majumbani kwao, badala yake wanakwenda kwa wanaume kuishi nao kama mke na mume.”
Mwalimu Ruchengura alisema kuwa, kwa mwaka 2013 alisajili wanafunzi wa kidato cha kwanza wapatao 472 wakati waliofaulu kwenda kidato cha kwanza walikuwa wachache tu.
Anatoa mfano kwa kusema kuwa wanafunzi waliotakiwa kufanya mtihani wa kumaliza mwaka ni 472 lakini si wote walioweza. “Wanafunzi 39 hawakufanya mtihani na miongoni mwao wanafunzi wa kike walikuwa 22.”
Aidha anasema kuwa kwa kidato cha nne walianza wanafunzi 306 lakini kati ya hao waliofanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne walikuwa 190 tu katika shule hiyo.
“Uelewa duni wa wazazi juu ya umuhimu wa elimu ndio tatizo kubwa linalochangia utoro wa wanafunzi, wazazi wanatakiwa kuelewa kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha wa mtoto na sio kumuacha anakwenda kuolewa au kuishi na wanaume wakati yuko shuleni,”alisema Mwalimu Ruchengura.
Kulingana na utafiti uliofanywa na chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), watoto 32, 161 walipata mimba na kukatiza masomo mwaka 2012.
Pendo John ambaye ni mwanafunzi wa darasa la 4 katika Shule ya Msingi Ushirombo wilayani Bukombe ni miongoni mwa wasichana walioshindwa kuendelea na masomo.
“Rafiki yangu wa kiume ambaye alikuwa fundi cherehani kila mara alikuwa ananipa Sh. 500 za kununua mihogo shuleni. Nilipokuwa nikitoka shuleni nilikuwa nakwenda nyumbani kupiga stori na mara kadhaa tuliishia kufanya mapenzi. Sasa nimeacha kwenda baada ya kujigundua kuwa nina ujauzito wa miezi 5,” anasema Pendo.
Hivi sasa Pendo mwenye umri wa miaka 13 bado anaendelea kwenda shuleni kusoma kwani walimu wake bado hawajagundua iwapo mwanafunzi wao tayari ni mjamzito. “Ninajificha sana ninapokuwa darasani ili mwalimu asijue kama nina ujauzito,” anasema kana kwamba hajui kwamba si jambo linalowezekana kwa mtu kuficha ujauzito kwani siku si nyingi utagundulika.
Anasema kuwa hali duni ya mama yake ndio chanzo cha yeye kupokea pesa kutoka kwa fundi cherehani. “Baba alitutelekeza nikiwa na miaka 8. Alikwenda kuchimba dhahabu lakini mpaka sasa nina miaka 13 hatujamuona nyumbani, tunaishi maisha ya kubahatisha,” anasema Pendo huku akilia kwa uchungu.
Kabla ya kupata mimba, Pendo anasema kuwa alikuwa na ndoto ya kuwa muuguzi. Hata hivyo, ndoto yake hiyo huenda isitimie kwani hata mwanamume aliyempa ujauzito amekwisha kimbia kukwepa mkono wa sheria. Kwa kukimbiwa na mpenzi wake inamaanisha kwamba atalea mimba na pengine mtoto atakayezaliwa peke yake.
Mariam Michel ni mama mzazi wa Pendo, anasema kuwa kama ilivyo kwa wasichana wengi wanaopata mkasa wa kupata ujauzito kienyeji, mwanawe alimficha kama alikuwa na mimba. “Kila anaporudi shuleni alikuwa anapenda kulala tu, ninapomhoji kwa nini unalala anasema amechoka na masomo!”
“Mie ni mtumishi wa Mungu niliota usiku kuwa mtoto wangu ana mimba kubwa na bwana aliyempa mimba amekimbia. Nilipoamka nikamchukua Pendo mpaka hospitali kupimwa na aligundulika ana mimba ya miezi sita,” anasema Mariam.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dk. Honorata Timisibwa anasema kuwa mimba za utotoni kwa mwaka jana katika Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita zilikuwa 3,142 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Novemba.
Dk.Timisibwa alisema kuwa tatizo kubwa la kuwa na watoto wengi wanaobeba mimba wakiwa na umri mdogo, ni kutokana na ugumu wa maisha pamoja na wazazi kutojali familia zao hasa mabinti wadogo ambao wengi wao wapo shuleni.
“Wazazi wanatakiwa kuwalea vema watoto wao na kuwaeleza juu ya madhara ya kujiingiza katika mapenzi,” anasema Dk. Timisibwa na kuongeza kuwa vinginevyo watoto wanapata mimba wakiwa bado wako shule za msingi.
Selina Martin ni mzazi wa mtoto Editha Mabula wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ushirombo. Mwanafunzi huyo hajaonekana nyumbani kwa muda mrefu na inadaiwa kuwa amekwenda kuishi na mwaume Kahama.
Selina alisema kuwa likizo ilipofika mtoto wake hakuonekana nyumbani ndipo alipotoa taarifa kwa ndugu zake kumtafuta binti yake lakini hakufanikiwa kumpata. “Nasikia tu kutoka kwa wanafunzi wenzake kuwa mtoto wangu kutoroka shule na kwenda kuishi na mwanaume,” anaongea kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi.
Theresia ni rafiki yake na Editha na anasema kuwa ni kweli rafiki yake yuko kwa mwanaume huko Kahama. “Ni kweli Edita yupo kwa mwanaume na sasa ana mimba.” Mwanaume anayeishi na Editha inaelezwa kuwa anafanya kazi katika machimbo ya dhahabu.
John Maziku ni mkazi wa Bukombe alisema kuwa, utoro kwa wanafunzi a shule za sekondari na msingi ni tatizo sugu katika wilaya hiyo, sababu kubwa ya kuwepo kwa utoro ni wazazi kutokuwa karibu na watoto wao.
“Wazazi wengi wanakwenda migodini wanakaa huko muda mrefu na hawakumbiki familia na anabaki mama na mzigo mkubwa wa kutunza familia.
“Wazazi ndio chanzo kikubwa cha utoro katika wilaya ya Bukombe kwa sababu baba anapokwenda kwenye machimbo ya migodi hakumbuki kuwa nyumbani ameacha familia na inatakiwa kuhudumiwa, hapo ndipo watoto nao wanaacha shule kwa kwenda kutafuta pesa.”
“Iwapo wazazi wangekuwa wanajali familia kwa kutuma huduma za matibabu na chakula watoto wangepata muda wa kwenda shule kusoma,” alisema Maziku.
Mwajuma Mohamed (15) mkazi wa Ushirombo amekatiza masomo yake akiwa darasa la sita baada ya kupewa mimba na dereva wa magari makubwa. Hivi sasa ana mtoto wa miezi 7 lakini baba yake hajawahi kupeleka huduma ya mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA, Valeriea Msoka anasema kuwa wamefanya kampeni ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondai na msingi juu ya umuhimu wa elimu na madhara ya mimba za utotoni.
Msoka alisema kuwa elimu hiyo imetolewa katika wilaya kumi ya mikoa ya kusini Lindi na Mtwara, Pwani pamoja na Dar es Salaam kupitia mradi wa GEWE ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (Danida).
“Elimu iliyokuwa inatolewa kwa wanafunzi ililenga juu ya kumwezesha mwanafunzi namna ya kujitambua na kujua elimu anayoisoma.”
Anasema mafunzo hayo ni kitu cha muhimu na yatachangia maendeleo ya mwanafunzi hapo baadae. “Hata kama wazazi wanapomlazimisha kuolewa binti anatakiwa kukataa ili aweze kumaliza elimu yake vizuri,” anasema Msoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles