32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Usiri wasababisha wajawazito kujifungulia nyumbani


DERICK MILTON -BARIADI

SERIKALI imesema kukosekana usiri katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, hasa maeneo ya vijijini, kumesababisha wajawazito wengi kujifungulia nyumbani.

Kutokana na hilo, vifo vingi vya wajawazito na watoto wachanga vilitokea kwa wingi kutokana na kutokwa kwa damu nyingi wakati wa kujifungua huku wakikosa huduma zinazostahili.

Hayo yalibainishwa juzi na mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Dinna Atinda, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama katika Mkoa wa Simiyu.

Dk. Atinda alisema zahanati nyingi za vijijini zilikuwa hazina sehemu za kuwekwa kina mama kujifungua na kufanya baadhi kujifungulia sehemu za kuhudumia wagonjwa wengine.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanawake wengi walikuwa wakiona aibu, hivyo kuamua kutokwenda kujifungulia vituoni badala yake kujifungulia nyumbani na kusababisha vifo.

“Baada ya Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo UNFPA, tumewezesha kujenga na kukarabati zaidi ya vituo vya kutolea huduma za afya 375, na katika Mkoa wa Simiyu ni 38 ambapo kati ya hivyo 21 ni zahanati, vituo vya afya sita na hospitali mbili,” alisema Dk. Atinda.

Alisema vituo hivyo vimeboreshwa na kutengwa sehemu za kina mama kujifungulia, hali ambayo imeongeza usiri na kusababisha idadi kuongezeka.

“Usiri umeongezeka, vituo hivi ambavyo tumeboresha tumefanikiwa kujenga wodi za wajawazito, kuwekwa huduma za msingi na dharura, tumetembelea Zahanati ya Mwasinasi Simiyu wameongezeka kutoka 20 kila mwezi hadi 80 na wote wanajifungua salama,” alisema Dk. Atinda.

Kwa upande wake, mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Dk. Hashina Bergan, alisema ili kuweza kupunguza vifo vya kina mama na wajawazito ni lazima kuboreshwa kwa mfumo wa uuguzi na ukunga.

Alisema wakunga wataalamu wana uwezo wa kutoa huduma bora za afya ya uzazi zinazojumuisha utunzaji wa mama na mtoto katika kipindi chote cha ujauzito hadi kufikia zaidi ya asilimia 87.

“UNFPA mbali na kuboresha sehemu za kutolea huduma za afya, tumekuwa tukisaidia katika hili kwenye nchi zenye uhaba mkubwa wa wakunga, hasa Tanzania, ambapo kwa Mkoa wa Simiyu tumewapatia mafunzo wakunga 378,” alisema Dk. Bergan.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa, Majeda Kihulya, alisema Mkoa wa Simiyu umepunguza vifo vya wajawazito kutoka 43 mwaka 2015 hadi 40 mwaka 2018 huku watoto wachanga vikiongezeka kutoka 488 hadi 494 katika kipindi hicho.

Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, aliwataka wataalamu wa Idara ya Afya ya Mkoa na halmashuari, kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles