29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kikwete ahofia migogoro ya ardhi Chuo cha Afya

PENDO FUNDISHA-MBEYA

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete amesema eneo la ardhi linalotarajiwa kujengwa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi   Mbeya linapaswa kufanyiwa upembuzi yakinifu kabla ya ujenzi huo kuanza  kuepuka migogoro na changamoto zisizo na tija.

Alisema  maeneo mengi ya ujenzi wa miradi mikubwa   nchini yamekuwa yakikumbwa na changamoto mbalimbali lakini kubwa ni migogoro ya wananchi wanaoyazunguka hivyo kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati.

Kikwete aliyasema hayo jana baada ya kutembelea na kukagua eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 3000 lililopo eneo la Tanganyika Packers  lililotengwa na serikali ya Mkoa wa Mbeya kwa ujenzi wa chuo hicho.

Kikwete alisema chuo kinahitaji eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa majengo lakini kama upembuzi yakinifu hautafanyika huenda hatua hiyo isifanikiwe kwa muda muafaka kutokana na muda mwingi kutumika katika kutafuta muafaka na utatuzi wa changamoto zitakazojitokeza.

“Ninakuagiza Makamu Mkuu wa chuo kufanya utafiti wa kutosha wa eneo hili, kweli ni kubwa na zuri, lakini nikiangalia hapa tupo karibu na kiwanda cha saruji, kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe na Mto Mbalizi, hivyo ninaomba tujiridhishe kwanza, isije tokea kama yale ya ujenzi wa chuo cha Mloganzila,”alisema.

  Rais huyo mstaafu alisema  Serikali imeamua kuwekeza katika sekta ya afya hususan   kwenye idara ya wataalamu kwa sababu  takwimu zinaonyesha   uhaba wa madaktari bingwa katika hospitali za mikoa ni asilimia 77, Rufaa na Kanda ni asilimi 53 hivyo mwaka 2012/2013 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilianzisha mafunzo ya udaktari na wauguzi lakini 2017/2018 yalisimamishwa.

“Mafunzo hayo yalisimamishwa kwa sababu mbalimbali  lakini sasa Rais John Magufuli, ameelekeza chuo hiki kuanza kutoa tena mafunzo haya na ameelekeza kutolewa Mbeya.

“Hivyo Amiri Jeshi Mkuu akiagiza linalofuata ni utekelezaji na ndiyo huu tunaufanya lakini lazima tahadhari ichukuliwe,” alisisistiza Kikwete na kuongeza:

“Awali CCM iliponipa dhamana ya kupeperusha bendera yake changamoto hiyo ilikuwapo na niliunda timu ya ushauri ambayo ilieleza kwamba moja ya changamoto inayoikabili sekta hiyo ni upungufu wa wataalam wa afya kwa vile  kwa kipindi hicho daktari mmoja wa Tanzania alikuwa akihudumia watu 30,000 na nesi akihudumia watu 25,000”.

  Kikwete alisema hiyo ndiyo sababu kubwa iliyosababisha Serikali ya sasa kuridhia na kutoa kibali cha chuo hicho kutoa mafunzo ya afya na sayansi shirikishi na kusisitiza kutolewa Mbeya ambako kwa sasa kinatumia majengo ya Hospitali ya Rufaa Kanda za Nyanda za Juu Kusini, kikiwa na   wanafunzi 1,146 na watumishi 85.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles