ELIUD NGONDO- MBEYA
WANANCHI wa Kijiji cha Kikondo, Kata ya Ilungu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia mgogoro kati ya kijiji chao na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo uliodumu kwa zaidi ya miaka 50, huku wakidai kunyanyaswa na kuporwa haki zao.
Pia wamelilalamikia jopo la makatibu wakuu wanane waliofika kijijini hapo hivi karibuni kutekeleza agizo la Rais la kumaliza migogoro ya hifadhi za taifa na vijiji 366 nchini.
Wananchi hao wamedai kuwa makatibu hao walitoa taarifa za kupotosha kupitia vyombo vya habari kwa kusema hakuna mgogoro.
Wakizungumza na MTANZANIA kijijini hapo hivi karibuni, wananchi hao walisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi na mwaka 2015 Rais Magufuli alipokuwa kwenye kampeni aliahidi kuumaliza mapema.
Katibu mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kijiji hicho, William Mponela, alisema mgogoro huo ulianza mwaka 1965 Serikali ilipokuwa inaanzisha shamba la mifugo na kuchukua maeneo yao bila kuwalipa fidia.
“Wakati huo wakazi wa eneo hilo walikuwa 26 na Serikali iliahidi kuwalipa fidia ambayo ilikuwa haizidi senti tano, lakini haikutekeleza hivyo wananchi hao wameendelea kuongezeka na sasa ni zaidi ya 2,000 hivyo fidia hadi sasa imefikia Sh bilioni 1.8.
“Mwaka 2007 Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) walianza kubomoa nyumba zetu bila kutulipa fidia na eneo lenyewe lina urefu wa kilomita 1.4. Tunamwomba Rais atusaidie ili waturejeshee eneo letu maana hakuna wanachofanyia na sisi hatuna eneo la kulima,” alisema Mponela.
Aidha Mponela alisema mbali na kulima, hawana eneo la kutosha kujenga wala kuchungia mifugo kwa kuwa ikiingia kwenye eneo hilo inakamatwa na wanatozwa faini isiyopungua Sh 100,000 kwa kila mfugo.
Mkazi wa kijiji hicho, Agape Swalo alisema walianza kupata matumaini ya kurejeshewa eneo lao baada ya Rais kutangaza kuwa vijiji vyote 366 nchini ambavyo vilikuwa vinadaiwa kuwa vipo ndani ya hifadhi visiondolewe.
Alisema matumaini yao yalianza kufifia baada ya jopo la makatibu wakuu kutembelea kijijini hapo bila kuwashirikisha ili kupata taarifa badala yake taarifa iliyotolewa ni kuwa hakuna mgogoro isipokuwa kijiji kipo kwenye chanzo cha Mto Ruaha.
Hivi karibuni makatibu wakuu wanane wa wizara tofauti wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dorothy Mwanyika, walieleza kuwa kijiji hicho kipo kwenye chanzo cha Mto Ruaha na hivyo wananchi wanatakiwa kuondolewa.