30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

JPM afyekelea mbali kikokotoo

AGATHA CHARLES, GRACE SHITUNDU Na PETER FABIAN-MWANZA/DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, ametangaza kikokotoo kilichotumika kwa kila mfuko kabla ya mifuko ya hifadhi za jamii haijaunganishwa na kuwa miwili kiendelee katika kipindi cha mpito hadi mwaka 2023.

Pia ametoa maagizo manne kwa wenyeviti pamoja na watendaji wakuu wa mifuko ya hifadhi ya PSSSF na NSSF, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kusimamia mchakato wa kuhakiki majina ya wastaafu ili kupata wastaafu hewa.

Kauli hiyo aliitoa Ikulu, Dar es Salaam jana katika kikao chake na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), watendaji, wakuu wa mifuko ya hifadhi za jamii na SSRA.

“Kustaafu si dhambi, kustaafu ni heshima, mtu anapofanya kazi yake hadi anastaafu ile ni heshima, lazima aheshimike. Kama kuna mwalimu amefundisha kuanzia darasa la kwanza amefanya kazi hadi anastaafu halafu apewe tena masharti kuwa tunakupa asilimia 25 mkupuo, kuwa zitakusaidia zingine ukiwa unaishi ulijua kama ninaishi.

“Wakati ninaziona fedha zangu nilizoweka kule unazalisha miradi ambayo haiishi. Sasa sifahamu nisemeje. Ninafahamu wanavyoona kuwa tukipinga kwa nguvu kubwa mifuko haitaishi lakini kama hii mifuko ikibadilika mwelekeo matumizi yakawa mazuri itaishi,” alisema.

Kutokana na hilo, aliamua kuwe na kipindi cha mpito hadi 2023.

“Nimeamua kikokotoo kilichokuwa kinatumika kwa kila mfuko kabla ya mifuko kuunganishwa yaani PSPF, GEPF, LAPF, PPF na NSSF kiendelee katika kipindi cha miaka ya mpito hadi mwaka 2023, nimepiga hesabu wanachama 58,000 ndio watastaafu katika kipindi hicho,” alisema.

Magufuli alisema anawapenda wafanyakazi hivyo hataki kuwachanganya na kikokotoo hicho kwa sababu kila mfuko ulikuwa na fomula yake.

Pia alisema walimu walikuwa na kikokotoo cha asilimia 50 hivyo wataendelea nacho na si asilimia 40 ambazo awali wachangiaji waliomba.

Alisema katika kipindi hicho mifuko itatengemaa na kuimarika zaidi na hata uangalizi utakuwa mkubwa na baadaye kutafutwa fomula nzuri wakishirikishwa wawakilishi wa wafanyakazi.

“Mimi nitaichungulia kweli kweli hiyo mifuko, waziri na katibu mkuu wa wizara husika wachungulie watu wasitumie kwa manufaa ya ovyo,” alisema.

MAAGIZO MANNE

Agizo la kwanza aliitaka mifuko ya jamii kupunguza matumizi aliyoyaita ya ovyo.

“Hifadhi za jamii zina matumizi ya ovyo, tutazungumzia fomula kumbe tatizo lipo hifadhi za jamii zenyewe,” alisema na kuongeza:

“Kama fedha zilipelekwa kujenga Ndege Village, mtu akitaka kuchukua mkopo wake hataukuta. Utakuwa umewekewa katika uwekezaji ambao hauzalishi na nyingi hazizalishi lakini wanazipenda kwa sababu wana masilahi huko.

“Mfano nafahamu kuna hifadhi ya jamii moja inatumia shilingi bilioni 1.3 ya kalenda, matangazo na udhamini kwa mwaka. Pia imeajiri walinzi wa gharama wanawalipa shilingi bilioni mbili kwa mwaka na kama wangeajiri Suma JKT wangelipa chini ya shilingi bilioni moja kwa mwaka.”

Agizo la pili aliitaka mifuko yote kuhakiki daftari la wastaafu.

“Sasa mimi niwaombe katika mifuko, waboreshe daftari la wastaafu ili kuondoa wastaafu hewa au kujiandikisha mara mbili.

“Kwa sababu nina uhakika kama tumekuwa na wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa, pembejeo hewa, mishahara hewa, hatuwezi kukosa wastaafu hewa. Lazima tunao. Au wastaafu walioandikwa majina mara mbili,” alisema.

Agizo la tatu alilolitoa lilihusu uwekezaji usio na tija kama ule wa Ndege Village kwa sababu haufai bali unawafaa watu binafsi.

Huku agizo la nne likiwa ni kupunguza gharama za uendeshaji wa mifuko ya kijamii kwa sababu imebaki miwili hivyo hakuna ushindani na kila mmoja ana wanachama wake hivyo sheria ifuatwe.

Pia alizitaka hifadhi hizo kushughulikia kuongeza wanachama wapya kwa sababu haoni ni kwanini NSSF iwe na wanachama 448,000 nchi nzima wakati sekta binafsi inasambaa kila mahali.

Alisema ni lazima kuangalia mapendekezo ya wanachama wakiwamo wa sekta ya ujenzi ambao hufanya kazi kwa vipindi mfano miezi 36 kisha wanamaliza kazi.

“Haiingii akilini nimefanya kazi hapo nikiwa na miaka 30 nisubiri hadi 60 ndipo nichukue michango yangu kwa sababu hakuna atakayenikumbuka hata mkandarasi atakuwa kaondoka,” alisema.

Alitolea mfano wafanyakazi wa Mgodi wa Tulawaka na ujenzi wa Stiegler’s Gorge.

“Kwanini katika uanachama wenu kusiwe na vipengele lakini kunakuwa na masharti kuwa atakayefikia miaka 60 anafaidika zaidi na fomula yake ni tofauti halafu huyo wa miaka minne fomula yake inakuwa ya aina fulani ili kupata wanachama wengi zaidi na mifuko idumu,” alisema.

Pia alisema alipowasikiliza wawakilishi hao wapo waliopendekeza kikokotoo hicho kubaki na asilimia 50 kama ilivyokuwa wamezoea kwa baadhi ya mifuko ya pensheni na hata walioko chini inafaa ipande.

Alisema wapo pia waliosema fomula ya kikokotoo inachanganya wafanyakazi kwa sababu walikuwa na malengo yao kutokana na kufanya kazi kwa uadilifu.

“Inapofika hapo hata hesabu hazieleweki nayo inasikitisha. Lakini kitu ambacho kipo mishahara ya sekta binafsi ni rahisi kucheza nayo, mtu anaweza akafika mwishoni akasema niwekee mshahara wa shilingi milioni 10 ili kukokotolewa kwa fomula iliyopo lakini Serikali si rahisi,” alisema.

Pia alisema hata waliokuwa na mishahara ya Sh milioni 20 hadi Sh milioni 25 ilishushwa na kufikia Sh milioni 15.

“Mishahara mingi ya wafanyakazi serikalini si mizuri sana, sasa anapofika tena mwishoni kile kikokotoo unampa kidogo kidogo, unasema atakuwa anapokea kidogo kidogo hadi atakapokufa, si nipe sasa hivi halafu nikafe potelea mbali si ni zangu.

“Nilipokuwa nachangia hukuniambia leo nimemaliza nataka nichukue mzigo wangu nikafanya shughuli yangu unaniambia wewe kaa tu hadi utakapokufa polepole napo maana haiingii kwa mtu yeyote,” alisema.

Pia alisema hata waliotayarisha suala hilo la kikokotoo mfano waziri akimaliza ubunge wake atapewa fedha zake hivyo akipewa asilimia 25 hawezi kukubali.

Alisema mfano PSPF Serikali inapeleka Sh bilioni 126 kila mwezi mbali na kulipa mishahara ya Sh bilioni 560.

Alisema fomula iliyokuwa inatumiwa na PSPF na LAPF haipo ya mtu anamaliza halafu kiwango kinazidishwa mara nne.

“Ninafahamu walioiweka fomula hiyo ni makatibu wakuu wa wakati ule si wakati wangu, walijua wao ni wanachama ili kupata kilicho cha juu, ni kosa walifanya. “Hawa watendaji mfano wa LAPF na PSPF hawawezi kuuliza kwa kuwa ni mabosi wamefanya,” alisema.

Pia alisema kustaafu ni heshima na kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa ni kujitoa kwa ajili ya kazi yako.

“Ukifanya kazi hadi kustaafu maana yake umefanya kwa uadilifu mkubwa. Ulianza labda na miaka 20 au 30 hadi ukafika 60 maana yake umejitoa ni heshima. Sasa unapoona hiyo heshima mwishoni inakuwa karaha, inakuwa kama mateso inachanganya, ni kwa mfanyakazi yeyote, mtu yeyote. Na mimi nataka niwaeleze, siko hapa kumchanganya mfanyakazi yeyote,” alisema.

Pia alisema hata yeye alikuwa mfanyakazi hivyo anafahamu hayo kwa sababu alipokuwa mwalimu alianza na mshahara wa Sh 1,045 mwaka 1981-1982.

“Sasa nifanye kazi nifikie kustaafu halafu inakuwa shida kupata hizo fedha zinisaidie pale ambapo pana upungufu napo inakuwa si vizuri. Ndiyo maana niliamua kuwaita niwe mwamuzi,” alisema.

Magufuli aliyesikiliza pande zote kuanzia ule wa SSRA, Serikali na wawakilishi wa wafanyakazi, kabla ya kuchukua uamuzi huo alielezea historia ya jambo hilo.

Alisema Oktoba 20, 2017, Baraza la Mawaziri lilipitisha uamuzi wa kuunganisha mifuko minne ya pensheni na kuwa mmoja kwa upande wa utumishi wa umma huku ule wa NSSF ukitakiwa kuendelea na kufanyiwa marekebisho.

Alitaja mifuko hiyo iliyounganishwa kuwa ni PSPF, PPF, GPF na LAPF ili kuunda mfuko mmoja wa watumishi wa umma huku NSSF ikibaki kuwa mfuko wa wafanyakazi wa sekta binafsi na zile zisizo rasmi.

Alisema Januari 31, mwaka huu Bunge lilipitisha Sheria ya PSSSF.

Alisema kabla ya mifuko kuunganishwa kila mfuko ulikuwa na wanachama (katika mabano) wake kama ifuatavyo, PPF (300,000), NSSF (442,729), GEPF (67,350), LAPF (173,779), PSPF (342,799) hivyo jumla kuwa 1,261,200.

Alisema katika watumishi wa sekta binafsi, mwajiri huwa anachangia asilimia 10 na mwajiriwa asilimia 10 huku upande wa serikalini ikitoa asilimia 15 kwa watumishi wa umma na mwajiriwa wake akitoa asilimia tano.

Alisema wakati anaingia madarakani, mifuko yote ya jamii ilikuwa na hali mbaya kutokana na yote mitano haikuwa kitu kimoja.

“Waendesha mifuko yote walikuwa wanapigana vita, walikuwa wanagombania wanachama, walikuwa hawapendani na wote walikuwa ndani ya Serikali. Kila mmoja alikuwa anataka wanachama walikuwa wanaweka matangazo. Kutokana na hilo kukawa na mchanganyo wa Serikali wako NSSF, wa sekta binafsi wako PPF, kila mahali,” alisema.

Alisema ipo mifuko iliyokuwa ikiendeshwa kiajabu kwa kuanzisha miradi ya majengo ambayo wapo waliopata asilimia 10.

Alisema alipoingia madarakani alikuta deni ambalo Serikali ilidaiwa kiasi cha Sh trilioni 1.2.

Pia alisema waliokuwa wakistaafu wakati ule ilikuwa ni shida kwa kuwa michango ilikuwa haipelekwi na ilibidi kuanza kukusanya makusanyo ya ziada kutoka Sh bilioni 800 hadi Sh trilioni 1.3 pamoja na kutoa watumishi hewa.

Alisema hadi Machi, mwaka jana  madeni yote yalikuwa yamemalizika ambapo ZSSF Sh milioni 135.8, PSSF Sh bilion 638.5, LAPF Sh bilioni 221.3, NHIF Sh bilioni 200.6, GEPF Sh bilioni 44.0, PPF Sh bilioni 41.5, NSSF bilioni 26.0 na WCF Sh bilioni 17.7 na kufanya jumla ya Sh trilioni 1.23.

Pia alisema hadi Agosti mosi, mwaka huu, idadi ya wastaafu wa PSSF walikuwa 8,000 na walikuwa wanadai Sh bilioni 740 na tayari Sh bilioni 550 zimelipwa na zilizobaki kabla ya Januari, mwakani zitakuwa zimelipwa.

Alisema NSSF watu wenye madai mbalimbali wanafikia karibu 16,000, waliokuwa wanadai 12,000 wamelipwa zaidi ya Sh bilioni 85 na waliobaki wanashughulikiwa waweze kulipwa.

Pia aliwataka wanasiasa kuacha kuingilia mifuko na hivyo atakayejipendekeza kwa wanasiasa atamwondoa.

Awali, wawakilishi wa wafanyakazi walitoa maoni yao huku baadhi wakiomba ifikiwe kikokotoo cha asilimia 40.

Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu, Jenista Mhagama, alisema walipanga kukutana na wawakilishi hao tena Januari, mwakani baada ya kutokubaliana.

RAIS TUCTA

Kwa upande wake, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana alisema wamefurahishwa na uamuzi wa Magufuli kwa sababu umewasaidia wafanyakazi ambao ndio wanyonge.

Alisema Magufuli amewapa wafanyakazi walichokuwa wanakitaka.

“Tumefurahishwa na uamuzi wa Rais kwa sababu hatua iliyokuwa imefikia ilihitaji uamuzi wake, ametupa wafanyakazi tulichokuwa tunakitaka” alisema.

BULAYA

Baada ya Magufuli kutoa tamko kuhusu kikokotoo hicho, Waziri Kivuli, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Esther Bulaya, aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter na kudai uamuzi huo ni ushindi kwa wafanyakazi.

“Hongereni wafanyakazi tulishikamana tushikamane tena kudai haki yenu ya nyongeza za mishahara na kupandishwa madaraja. Mungu awabariki,” aliandika na kuongeza:

“Sasa Jenista na Mkurugenzi wa SSRA, mjiuzulu nimewashinda, hamkuwatetea wafanyakazi. Asanteni wafanyakazi tumeshindaa, sijawahi kushindwa, huwa nasimama kwenye ukweli.”

Bulaya ambaye pia ni Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) na wabunge wenzake wa upinzani walipinga kanuni hiyo mpya ya mifuko ya hifadhi ya jamii inayotamka kwamba mstaafu atalipwa asilimia 25 ya mafao na zilizobaki kulipwa kama mshahara kwa miaka 12.

ZITTO
Naye Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alimshukuru na kumpongeza Magufuli kwa kufanya uamuzi unaowasaidia wafanyakazi.

Akiandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, Zitto, alisema na kuongeza:

“Kutokana na uamuzi wa Magufuli kuhusu kikokotoo cha mafao ya pensheni kwa wastaafu, sisi ACT Wazalendo na vyama vya upinzani kwa ujumla tumesimama na wafanyakazi toka mwanzo wa sakata hili, wakati sheria ikiwa muswada na hata baada ya kanuni kutungwa.

“Kwetu, jambo lolote linaloongeza masilahi na ustawi wa wafanyakazi ni jambo jema na muhimu. Tunashukuru kuwa Magufuli ametuelewa na amekuja upande wetu na kuacha upande wa waziri wake, washauri wake na watendaji wa Serikali yake.

“Kwetu huu si wakati wa kunyang’anyana sifa. Washindi ni wafanyakazi na Watanzania. Tunapoelekea mbele, tunamwomba Magufuli asiwe na aibu kutusikiliza na mengine mengi kwa kuwa nia yetu ni njema tunajenga nchi moja.

“Rais Magufuli atusikilize pia kuhusu mishahara ya watumishi wa umma, atusikilize kuhusu mateso ya wadau wa korosho na atusikilize kuhusu muswada wa sheria ya vyama vya siasa. Kama hili la wafanyakazi hatukutumwa na mabeberu, basi na mengine pia hatutumwi na mabeberu.”

WAFANYAKAZI WAANDAMANA

MWANZA

Katika hatua nyingine, baadhi ya wafanyakazi taasisi mbalimbali za Serikali jijini Mwanza, waliandamana kupongeza uamuzi wa Magufuli wa kufuta kikokotoo.

Wafanyakazi hao waliandamana kutoka Viwanja vya Ghand na kupita Barabara ya Nyerere na Kenyatta na kuingia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.

Walisema wamefurahishwa na uamuzi wa kurejesha utaratibu wa zamani wa ulipaji wa mafao ya wastaafu.

Akizungumza na wafanyakazi hao, Mongela, alivipongeza vyama vya wafanyakazi kwa umoja wao na uamuzi wa kuandamana kumpongeza Magufuli kwa uzalendo wa kutetea masilahi ya wafanyakazi.

“Tanzania imeonyesha ni taifa tunalosikilizana, hivyo rai yangu ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuunga mkono kazi na uamuzi mzuri wa Rais na ombi langu vyama vya wafanyakazi tuendelee kuwa na umoja huu na kubwa zaidi tuendelee kumwombea na kuliombea taifa letu tufikie malengo,” alisema.

Katibu wa Tughe Mkoa wa Mwanza, Aloyce Mapembe, alipongeza uamuzi wa Magufuli na alisema wanauunga mkono.

Naye Katibu Msaidizi wa Tuico Mkoa wa Mwanza, Elvis Kissa, alisema uamuzi wa Magufuli kusikiliza kilio cha watumishi wastaafu walioanza kazi wakiwa vijana na kulitumikia taifa kwa nguvu na ari kubwa ni mzuri.

Naye Katibu wa TALGU, Odakis Stephani, alisema amekunwa na uzalendo na usikivu wa Magufuli wa kufuatilia hali ya wastaafu na amewaongezea maisha kwa kukataa kikokotoo kipya kutumika hadi wadau wote kukaa na kuona njia nzuri ya kufikia uamuzi mwingine mzuri.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Mwanza, Sibola Kisheli,  alipongeza kurejesha malipo hayo kwa wastaafu na walimu watafundisha kwa nguvu moja na wanao uhakika wa kustaafu na kupata mafao yao yatakayowasaidia kujikimu na kusomesha watoto wao. Naye Katibu wa Tucta Mkoa wa Mwanza, Yusufu Simbaulanga, alisema uamuzi wa Magufuli umewarejesha wafanyakazi katika furaha na kuwatoa katika majonzi waliyokuwa nayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles