27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Jay Dee aanika urithi alioachiwa na Oliver Mtukudzi


CHRISTOPHER MSEKENA

*Apewa hadhi ya ushujaa, Fid Q aongea yake

‘MWANAMUZIKI Mkubwa’, ndilo jina ambalo staa wa Bongo Fleva, Judith Wambura maarufu kama Lady Jay Dee, ameona linamtosha jabari la muziki barani Afrika, Oliver Mtukudzi, aliyefariki dunia Jumatano wiki hii huko, Harare Zimbabwe.

Jide ambaye alikutana kwa mara ya kwanza na Mtukudzi mwaka 2001 huko Sound City, Afrika Kusini katika tuzo za Kora, amekuwa miongoni mwa mastaa wengi duniani waliotuma salamu za pole kufuatia kifo cha mwanamuziki huyo kilichotokea katika kliniki ya Avenues alipokuwa akipatiwa matibabu ya Kisukari.

Mtukudzi (66), alikuwa ni mwanamuziki, mtunzi wa nyimbo, mtunzi na mwongozaji wa filamu, aliweza kuuweka kwenye ramani ya dunia muziki wa Afrika kupitia albamu zake zaidi ya 59 na nyimbo kubwa kama Lord, Hear Me, Todii na Neria zilizolenga kuwakomboa wanawake na watoto dhidi ya ukatili.

Jay Dee ameliambia Swaggaz kuwa miongoni mwa urithi ambao ameachiwa na Oliver Mtukudzi ni kuacha kutegemea kompyuta katika kuandaa na kutumbuiza muziki na kuwekeza nguvu kwenye muziki wa ala na vyombo ili kuutambulisha Uafrika.

“Nilikutana naye kwenye tuzo za Kora, yeye alikuwa anapafomu na  mimi pia nilikuwa napafomu, nikamfuata tukazungumza, tukabadilishana mawasiliano, tukawa tunawasiliana kwa ‘email’ kwa kipindi cha miaka kama saba mfululizo,

“Nilikuwa namuuliza, namwomba ushauri na mambo ya hapa na pale, akiwa kama mwanamuziki mikubwa aliyetutangulia na hatimaye mwaka 2011, wakati na mgahawa wa Nyumbani Lounge , nikaandaa onyesho ambalo nilimwalika, akaja tukapafomu pamoja, na hapo ndiyo tukapata nafasi ya kufanya wimbo wa pamoja (Mimi ni Mimi),” anasema Jay Dee.

Jide ambaye yupo mbioni kutumbuiza katika onyesho la  Valentine Februari 9 pale The Cask, Rock City Mall jijini Mwanza anasema: “Kitu ambacho Oliver  aliniambia na ninakizingatia mpaka leo, nilipompa albamu yangu ya kwanza ya Machozi, akaniambia unafanya muziki wa kompyuta, ili kutofautisha na kuonyesha Uafrika ni vizuri ukaingiza vyombo vya kama konga, magitaa na vitu vingine, baada ya hapo nikaingia kwenye muziki wa ‘live’ moja kwa moja,

“Jambo kubwa la kujifunza kutoka kwa Tuku ni kuwa wewe bila kujaribu kuwa mwingine na hii ni kutokana na aina ya muziki aliokuwa akiufanya, alishikilia ‘sound’ yake ya kiafrika na melodi za nyumbani ambazo zimempatia umaarufu na heshima kubwa duniani,” anasema Jide.

FID Q ASIMULIA MKASA WAKE NA MTUKUDZI

Miongoni mwa wasanii wa Tanzania waliobahatika kufanya kazi na Oliver Mtukudzi ni Fid Q, ambaye alikutana na nguli huyo nchini Msumbiji katika tamasha la kufunga na kufungua mwaka linaloitwa Umoja Cultural Flying Carpet.

Fid Q ambaye aliongozana na Chid Benz jijini Maputo, anasema wasanii wengi waliogopa kufanya shoo baada ya Oliver Mtukudzi, ili wasiwachukize mashabiki ambao mda mfupi uliopita walikuwa kwenye moto wa burudani uliowashwa na Tuku.

Hatua hiyo ilifanya uongozi wa tamasha kumfuata Fid Q, na kumwomba atumbuize baada ya Mtukudzi kukamilisha onyesho lake, jambo ambalo baadaye alijutia kwani alijikuta akitamani kurudisha mkwanja aliolipwa kutokana na uoga wa kukonga nyoyo za mashabiki sawa sawa na Oliver.

 “Nikamwita Chid kisha nikamwambia ‘aisee tutatoboa leo hapa’. ‘Chid akaniambia, kiukweli ni pagumu lakini ndiyo vile tena tushakula pesa ya watu, nikamwambia naweza kuwarudishia pesa yao kama vipi tupige chini hii kazi, Chid akaanza kucheka huku akiniambia,  acha wenge, cha msingi tujiandae kuwarapia sana, pesa hairudi hapa,

“Akaniambia nigonge ‘push up’ 10 ili woga unitoke, nikafanya hivyo, MC akautangazia umma kuwa anayefuata ni kutoka Tanzania, shangwe za ajabu zikasikika, wakati napanda jukwaani kuna nilipotajwa uwanja ulichangamka na tulianza na wimbo Agosti 13, tulifanya shoo ya kuwavutia watu wote waliohudhuria.”.

Anasema siku iliyofuata wakiwa wanapata kifungua kinywa alikutana na Oliver Mtukudzi ambaye alimfurahia na wakakubaliana kufanya kolabo mbili. Licha ya makubaliano hayo ambayo Fid Q alitakiwa kwenda Zimbabwe, mipango  ya kufanya kazi haikufanikiwa kutokana na ratiba zake nyingi jambo ambalo mpaka leo hii anajutia.

LINEX AIKOSA KOLABO

Mwanamuziki Sunday Mjeda ‘Linex’, amesema alikuwa mbioni kukamilisha kolabo yake ya Mtukudzi lakini kwa bahati mbaya haijaweza kufanikiwa baada ya kifo hicho kutokea.

“Nilikuwa nawasiliana na mtoto wake anaitwa Jackie, nilishamtumia biti na sauti yangu, ilibaki Mzee akingize sauti yake tu kisha mimi nimfuate Zimbabwe, tukafanye video nirudi nayo Tanzania, lakini ilishindikana kwa sababu alikuwa bize sana,” anasema Linex.

MENGINEYO KUHUSU MTUKUDZI

Enzi za uhai wake, Mtukudzi alibahatika kuwa na watoto watano na wajukuu wawili. Mwaka 2010, mtoto wake wa kiume  Sam, ambaye alikuwa mwanamuziki alifariki duniani kwa ajali ya gari wakati akitoka Norton kwenda Harare.

Pia Mtukudzi ambaye ni baba wa Afro Jazz, amejizolea tuzo nyingi za ushindani na heshima zaidi ya 24 kutoka ndani na nje ya Afrika. Hali kadharika juzi rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa alimtangaza Mtukudzi kuwa shujaa wa taifa, hadhi isiyo ya kawaida ambayo hutolewa kwa mtu asiyekuwa mwanasiasa.

Mtukudzi, anakuwa shujaa wa pili wa taifa la Zimbawe baada ya naibu kansela wa Chuo Kikuu Phineas Makhurane, aliyepewa hadhi hiyo Desemba mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles