LONDON, UINGEREZA
CHAMA cha kihafidhina cha Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kimepoteza viti vingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hapo juzi, baada ya jumla ya viti 1,335 kuchukuliwa na vyama vingine, huku shinikizo la kumtaka kiongozi huyo ajiuzulu likizidi kushika kasi nchini humo.
Shirika la Habari la Sky News limeripoti kuwa chama cha upinzani, Labour kinachoongozwa na Jeremy Corbin kilipoteza viti 86. Kwa upande wao, Chama cha Waandishi wa Habari kimesema haya ni matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi wa serikali za mitaa kuwahi kutokea tangu mwaka 1995 kwa chama kinachoongoza serikali kushindwa vibaya.
Chama cha Kiliberali kimepata ushindi mkubwa kwa kupata zaidi ya viti 700. Wachambuzi wengi na wanasiasa wanasema suala la Uingereza kujiondoa uanachama wake katika Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa sababu kubwa ya kushindwa vyama vikuu viwili nchini humo.