28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

USALAMA BARABARANI: SHERIA IMESAHAU VIZUIZI KWA WATOTO SAFARINI

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


OKTOBA 16 ni Siku ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani. Maadhimisho haya yalifanyika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo kilele chake ni kesho (Jumamos Oktob 21).

Wakati maadhimisho hayo yakifanyika mwaka huu yakiwa na ujumbe ‘zuia ajali okoa maisha’ bado kuna kilio kila kona kwa wadau mbalimbali wakihitaji marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani hasa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973.

Baadhi ya mambo ambayo yanapigiwa kelele kuzingatiwa katika marekebisho ni mwendo kasi, ulevi wakati wa uendeshaji, uvaaji kofia ngumu, kufunga mikanda na vizuizi kwa watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari (Tamwa), Edda Sanga anasema Sheria  ya usalama barabarani ya mwaka 1973 Kifungu cha 51(8) inatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi ni muhimu Sheria itamke maeneo yote na si yale ya mjini tu au makazi.

“Itamke wazi kuhusu maeneo ya shule, nyumba za ibada, maeneo ya michezo na mbuga za wanyama tofaut na ilivyo sasa,” anasem Edda.

Edda anasema kifungu cha 45 kinakataza mtu kuendesha gari akiwa amekunywa pombe zaidi ya kipimo kilichowekwa na sheria ambacho ni 0.08g/dl. Kiwango kinachotambuliwa na sheria yetu ni kikubwa kulinganisha na utafiti uliofanywa, kiwango kinachotambulika kimataifa ambacho ni 0.05g/dl kwa dereva mzoefu na 0.02 g/dl kwa dereva asiye mzoefu.

“Eneo lingine ni Kifungu cha 39(11) ambacho kinawataka madereva wote wa vyombo vya magurudumu mawili au matatu kuvaa kofia ngumu muda wote wanapoendesha chombo hicho. Sheria haitambui uvaaji wa kofia ngumu kwa abiria wa chombo hicho,” anasema Edda.

Anaongeza kuwa Kifungu cha 39 (11) kinamtaka dereva na abiria wa kiti cha mbele kufunga mkanda muda wote wa safari, sheria haijatamka chochote kuhusu abiria wa nyuma pamoja na watoto.

Anasema kuhusu vizuizi kwa watoto Sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 haijatamka chochote juu ya suala la vizuizi kwa watoto, hivyo mtoto hana ulinzi wowote akiwa kwenye chombo cha usafiri.

Anasema kutokana na idadi kubwa ya vifo na ajali barabarani ambavyo hutokea kwa kiwango cha kutisha nchini ipo haja ya kuchukua hatua madhubuti kukomesha ajali hizo.

Edda anasema  kuna umuhimu wa kuchukulia jambo hili kama dharura kwa kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni za usalama barabarni ili kuipa nguvu sheria hiyo kuwadhibiti wanaokiuka matumizi sahihi ya barabara.

Anasem takribani Watanzania 4,000 hufa kila mwaka kutokana na ajali za barabarani. “Takwimu zinasema kuanzia Januari hadi Julai, 2016;  watu 1580 walikufa kutokana na ajali barabarani, wengine 4,659 walijeruhiwa katika ajali 5,152 zilizotokea nchi nzima huku waliokufa kutokana na ajali za pikipiki wakiwa 430, waliojeruhiwa ni 1,147 katika ajali 1,356,” anasema Edda.

Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anasema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO),  zinaonesha Tanzania inaongoza kwa ajali za barabarani  kwa asilimia 33.

Anasema asilimia 74 ya wanaopoteza maisha wengi ni vijana hasa wanaume wenye umri kati ya miaka 18 hadi 29.

Samia anasema ajali hizo huchangiwa na uchovu wa madereva, mwendokasi, ulevi na utumiaji wa simu.

Anasema takwimu za WHO zinaonesha watu milioni 1.25 hufariki kila mwaka ambapo ajali za barabarani huathiri uchumi wa taifa kwa wastani wa asilimia tatu ya pato la taifa.

Anasema zipo sababu nyingi zinazochangia uwapo wa ajali lakini waendesha pikipiki wamekuwa wakivunja sheria za barabarani kwa makusudi.

Samia anasema mchango wa madereva wa bodaboda ni mkubwa lakini watambue hawapo juu ya sheria.

Anasema ni muhimu kwa kikosi cha usalama barabarani na baraza lake pamoja na wadau kubadilishana uzoefu na kuona namna ya kumaliza tatizo la ajali.

Samia anasema ni muhimu kuelekeza nguvu kudhibiti makosa matano mwendokasi, ulevi, kutokuvaa kofia ngumu, kutokufunga mikanda ya usalama katika gari na ukosefu wa vifaa vya kuwalinda watoto wadogo wakiwa kwenye gari.

Samia pia amewataka wananchi kujenga mazoea ya kutoa taarifa pindi wanapobaini kuna upungufu wakiwa katika usafiri.

Anasema baraza lihusike kikamilifu kusimamia na kuchochea uanzishwaji wa mfumo wa magari wa lazima ili kuhakikisha usalama wa magari yetu.

“Baraza liendelee kuishauri serikali matumizi ya teknolojia ya kisasa, ili kulinda maisha ya watu na mali zao,” anasema Samia.

Anasema anatambua uwepo wa madereva wenye leseni feki hivyo ifike wakati askari wakasimamia utoaji leseni ili kuwapata madereva bora.

Naye Ofisa Habari kwa umma wa Baraza la Ushauri Watumiaji Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatr CCC), Nicholous Kinyariri anasema kuanzishwa kwa vilabu shuleni kumechangia kukuza uelewa wa elimu ya usalama barabarani.

Anasema kama wadau bado wanaona abiria wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya sheria zilizopitwa na wakati jambo ambalo linachangi makosa kuzidi kuendelea.

Kinyariri anasema ubovu wa sheria hiyo ya mwak 1973  imekuwa ikichangia kuendelea kwa makosa.

“Mbali ya sheria kupitwa na wakati lakini ni fursa kwa wananchi kutambua haki na wajibu wao pindi wanapokuwa katika usafiri wa umma,” anasema Kinyariri.

Mwishoo

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles