NA WAANDISHI WETU
MATUKIO ya milipuko ya mabomu mkoani Arusha yametajwa kuwa ni njama za magaidi katika kuiathiri sekta ya utalii kama wanavyoendelea kufanya kwenye miji ya Zanzibar na Mombasa nchini Kenya.
Jiji la Arusha ndilo linaongoza kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, huku likitajwa kupokea idadi kubwa ya watalii kutokana na watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani kukimbia machafuko ya mara kwa mara nchini Kenya hasa kwenye mji wa Mombasa.
Hali hiyo inatajwa kuwaudhi wafadhili wa magaidi wanaojihusisha na biashara ya utalii nchini Kenya, ambapo wameamua kulivuruga soko la utalii kwenye maeneo yote yanayowavutia watalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Lengo la kutekeleza dhamira hiyo ni kuhakikisha soko la utalii nchini Tanzania linashuka sawa na ilivyo nchini Kenya.
Hatua hiyo ya kuvuruga soko la utalii jijini Arusha, inaonekana dhahiri kutokana na mfululizo wa utupaji wa mabomu unaolenga maeneo ya starehe ama makazi ya watu.
Kabla ya bomu lililotupwa juzi usiku kwenye mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine uliopo karibu na Viwanja vya Gymkhana na kujeruhi watu wanane, wahusika hao ambao bado hawajafahamika walirusha bomu nyumbani kwa kiongozi wa Taasisi ya Answar Muslim Youth Centre Kanda ya Kaskazini, Sheikh Sudi Ally Sudi.
Mtaalamu wa masuala ya biashara za utalii, Edward Selasini, alisema anaamini wanaorusha mabomu hayo wanatumia mbinu mbalimbali ili kulichanganya Jeshi la Polisi kuweka fikra kwenye jambo moja.
“Hawa jamaa wanatumia mbinu nyingi katika kuficha dhana ya kufifisha utalii na ndio maana wanarusha mabomu sehemu mbalimbali, lengo lao ni kuhakikisha wanavichanganya vyombo vya usalama, wakirusha kwenye mikutano ya siasa jamii itadhani ni masuala ya siasa, wakirusha kwa watu wa dini jamii itadhani ni masuala ya kidini, lakini ukweli nia yao ni kuwatisha watalii waamini Arusha haiko salama,” alisema.
Akizungumza na MTANZANIA Jumatano, Selasini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Connect Tanzania Serengeti Sarafi’s, alisema milipuko ya mabomu inayotokea Arusha ni njama za baadhi ya wafanyabiashara ya utalii nchini Kenya.
Alisema lengo lao ni kuhakikisha watalii hawafiki Arusha hali ambayo inaelekea kufanikiwa kwani kwa kiasi kikubwa ujio wa watalii umepungua.
“Watalii wamepungua, tayari wageni wangu sita waliokuwa waje nchini wamenitumia barua pepe ya kuahirisha safari yao bila sababu za msingi, hii ni hasara kubwa na sisi huku tayari tulikuwa tumeshajipanga kuwapokea, lakini haya yote yanasababishwa na mabomu ya mara kwa mara, hizi ni mbinu za kibiashara,” alisema.
Selasini aliongeza kuwa kama hali hiyo itaendelea, ipo hatari ya wageni wengi kufuta safari zao.
“Kule Kenya tumepata taarifa kutoka kwa washindani wetu wa kibiashara wanaitumia milipuko hii kama sehemu ya kujinufaisha wao, kwani wageni wanashukia pale Nairobi tayari kwa kuja Tanzania, baadhi wamekuwa wakiwapa taarifa kwamba huku kwetu kuna matukio ya ugaidi.
“Na kwa bahati mbaya dunia imekuwa kijiji siku hizi, hizi taarifa zinazoandikwa hapa nchini kwetu zinawafikia, wanajua kinachoendelea nchini kwetu. Sasa ipo haja ya wadau wanaohusika kukaa na kujipanga kwa dhati kukabiliana na hila hizi za wenzetu,” aliongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Utalii ya Tanzania Amazing Tours and Travel, Godfrey Owenya, alisema tangu milipuko ya mabomu ianze kutokea jijini Arusha mambo yamekuwa mabaya hasa kwenye sekta ya utalii.
Alisema kutokea kwa milipuko hiyo kumeendelea kuwafanya wateja wao kutoka nje ya nchi kukumbwa na hofu ya usalama wao.
“Kutokana na kuibuka kwa hali hiyo ni vema Bodi ya Utalii nchini (TTB) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakatumia maonyesho ya utalii yanayofanyika duniani kote kila mwaka kuielezea hali nzuri ya amani katika Jiji la Arusha,” alisema.
JESHI LA POLISI LAWASAKA WAHUSIKA
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu wanaohusika na utupaji wa mabomu.
Akizungumzia mlipuko wa bomu uliotokea juzi na kuwalenga watu wenye asili ya Asia wanaodhaniwa kuwa ni watalii, DCI Mungulu alisema mlipuko huo ulitokea juzi saa 4 usiku, ambapo kulikuwa na mkusanyiko wa watu waliokuwa kwenye mgahawa uliopo jirani na Viwanja vya Gymkhana ambavyo vipo karibu na nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Alisema bomu hilo lilirushwa na mtu asiyejulikana ambaye alifika kwenye eneo hilo na kufanya kitendo hicho na kukimbia.
Alisema mpaka sasa Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili wanaodhaniwa kushiriki kwenye tukio hilo na kwamba wanaendelea kuwahoji.
“Polisi inawashikilia watu wawili ambao tunadhani wameshiriki kurusha bomu hilo kwenye mgahawa ule na kujeruhi watu wanane ambapo mmoja wao ni mahututi,” alisema Mungulu.
Aidha, aliongeza kuwa tangu matukio hayo yaanze kutokea, tayari wameshakamata watu zaidi ya 20 wakiwemo sita ambao wamehusika kurusha bomu nyumbani kwa Sheikh Sudi.
CHADEMA HAINA USHAHIDI WA MABOMU
Kwa upande mwingine, DCI Mungulu amesema viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hawana ushahidi wowote unaohusisha mtu aliyelipua bomu mwezi Juni mwaka jana kwenye mkutano wao uliofanyika kwenye Viwanja vya Soweto jijini Arusha.
Alisema viongozi wa jeshi hilo walikaa kwenye kikao cha siri na viongozi wa Chadema ili kujadili suala hilo, lakini hakuna hata kiongozi mmoja aliyeleta ushahidi wa kutosha wa madai ya mtu aliyehusika kurusha bomu kwenye mkutano huo.
Jiji la Arusha limekuwa likikumbwa na milipuko ya mabomu mara kwa mara, mlipuko wa kwanza ulitokea Oktoba 25, mwaka 2012.
Wahusika walirusha bomu la kutengenezwa kwa mkono lililomjeruhi usoni, Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Arusha, Sheikh Hussein Jongo.
Wakati Jeshi la Polisi likiendelea kuwasaka walipuaji, Mei 5, 2013 katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti, bomu jingine lilirushwa na kusababisha vifo vya watu wanne na wengine 70 kujeruhiwa.
Juni 14, 2013 mlipuko mwingine ulitokea Viwanja vya Soweto ulipokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni za Chadema za uchaguzi mdogo wa kata nne za Themi, Elerai, Kaloleni na Kimandolu.
Katika mlipuko huo watu wanne walifariki na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa.
Aprili 13, mwaka huu watu hao wasiokamatika walitupa bomu jingine kwenye Bar ya Arusha Night Park na kujeruhi watu 17.
Mlipuko wa juzi ulikuwa ni muendelezo wa milipuko hiyo, kama ilivyokuwa kwenye eneo la Mpeketoni mjini Mombasa nchini Kenya,
Habari hii imeandikwa na Gabriel Mushi, Patricia Kimelemeta, Asifiwe George, Dar es Salaam na Eliya Mbonea na Janeth Mushi, Arusha