MWANDISHI WETU-MOSHI
WAFANYABIASHARA wa dawa za kulevya aina ya mirungi wamebuni mbinu mpya za kusafirisha dawa hizo kwa kutumia magari ya kifahari yakiwemo Toyota Land Cruser , Toyota Alphasad, Toyota Vanguard huku wengine wakilazimka kuzifanyia mabadiliko gari aina ya Toyota Noah ili kurahisisha ubebaji wa mirungi kwa kificho.
Hata hivyo tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limebaini mbinu hizo baada ya kufanikiwa kukamata gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 443 DET lililokuwa limebeba kilo 102 za mirungi likielekea Kondoa mkoani Dodoma.
Akizungumzia suala hilo jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hamis Issah alithibitisha kukamatwa kwa gari hilo saa 6:30 jioni katika kizuizi cha askari eneo la kwa wasomali likielekea njia ya Arusha.
“Tumeendelea na zoezi la kukamata wasafirishaji wa dawa za kulevya ,tumekamata kwa mara nyingine gari aina ya Noah, hili gari limetokea maeneo ya mkoani Kilimanjaro, linaelekea mkoani Dodoma katika Wilaya ya Kondoa.
“Hili gari limebadilishwa badilishwa ndani ukilitizama limejengewa vyumba maeneo tofauti tofauti kwa ajili ya kuwekea mirungi, bampa la mbele lina vyumba ,ndani kumetobolewa na kuchomelewa vizuri , yaani limefanyiwa mabadiliko makubwa kwa ajili ya shughuli hii ya usafirishaji wa mirungi, ukikagua kwa shaka huwezi gundua kwa mara moja,” alisema Kamanda Issah.
Alisema hadi sasa watu wawili wanashikiliwa huku akiwataja majina kuwa ni Simoni Boaa mkazi wa Babati na aliyekuwa dereva wa gari hilo na Abushir Abdallah mkazi wa Kondoa na kwamba taratibu zikikamilika watafikishwa mahakamani huku akitoa onyo kwa wafanyabiashara wa mirungi walioshindwa kuacha biashara hiyo .
“Kwa sasa mbali na kukamata tu hawa wasafirishaji ,tutaenda mbali zaidi kwenda kuangalia na mali zao hasa hizi zinaotumika katika usafirishaji ikibidi tushauri sheria ifanyiwe mabadiliko wasipate kabisa haya magari yao,” alisema Kamanda Issah .
Alisema katika kipindi kisichozidi siku 10 tayari yamekamatwa magari matatu likiwemo Toyota Alphasad lenye namba za usajili T 308 DMS lililokamatwa hivi karibuni likiwa na kilogramu 320 za dawa za kulevya aina ya mirungi likisafirisha kuelekea mkoani Arusha.
Kamanda Issah alisema tukio jingine la hivi karibuni ni lile la kikosi cha pikipiki cha jeshi hilo kilikamata kilogramu 80 za Mirungi iliyokuwa ikisafirishwa kwa kutumia pikipiki kutoka nchi jirani ya Kenya.
Kukamatwa kwa dawa hizo nyingine zinafanya idadi kamili ya dawa za kulevya aina ya mirungi zilizokamatwa hadi sasa kufikia kilo 502 pamoja na vyombo vya usafiri yakiwemo magari mawili na pikipiki moja.