27.7 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Maumivu yanayotokana na kuahirisha uchaguzi Nigeria

Wagombea urais Atiku Abukabari (kushoto) na Rais Muhammadu Buhari.

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

KATIKA siku waliyotarajia kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wao; rais na wabunge wa taifa, Wanigeria waliokata tamaa walilazimika kubadili mpango wao huo wa siku hiyo.

Ni kwa vile saa chache kabla ya upigaji kura kuanza, Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza uamuzi wa kuahirisha chaguzi hizo kwa wiki moja.

Kutokana na muda wa tangazo hilo saa nane usiku za Nigeria, mamilioni ya wapiga kura—hasa wale wasiofikiwa na intaneti pamoja na mitandao ya jamii walikuja kubaini hilo wakati walipoamka wakiwa wanajiandaa kwenda vituoni, asubuhi ya siku hiyo ya Jumamosi ya Februari 16.

Kuna ripoti ya baadhi ya watu kupanga foleni mapema kabla ya kujikuta kwa mshangao wa kutoamini wanachoambiwa kuwa uchaguzi huo haupo siku hiyo.

Sasa uchaguzi wa Rais na Bunge la Taifa utafanyika mwishoni mwa wiki hii, Jumamosi ya Februari 23 huku zile za ugavana na wabunge wa majimbo zikiwa pia zimesogezwa hadi Machi 9 badala ya tarehe ya awali ya Machi 2.

Macho na masikio ya wengi yalielekezwa kwa uchaguzi wa rais wenye ushindani mkali miongoni mwa wagombea wakuu wawili; Rais Muhammadu Buhari na Makamu Rais wa zamani Atiku Abubakari.

Ni uchaguzi unaokumbushia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wakati Tume Huru ya Uchaguzi (CENI), ambayo licha ya changamoto lukuki ikiwamo kuunguliwa kwa maghala yake ya kuhifadhi vifaa vya kura, huku vingine vikiwa bado kuwasili iliwahakikishia Wakongo kuwa uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa Desemba 23, 2018.

Lakini ikiwa zimebaki siku chache tu ikatangaza kuahirisha hadi Desemba 30 kwa sababu hizo za mchewesho licha ya awali kudai lije jua au mvua msamiati wa kuahirisha haupo!.

Nchini Nigeria, Mwenyekiti wa INEC, Mahmoud Yakubu, ndiye aliyetangaza uamuzi huo, ambao pia ulipingana na ule wa mara kwa mara uliowahakikishia Wanigeria na waangalizi wa kimataifa kuwa timu yake imejiandaa kikamilifu kuendesha uchaguzi huo.

Tume ilieleza kuwa sababu ni za kilojistiki na uendeshaji hasa baada ya kuunguliwa kwa ofisi zake na kuchelewa kwa vifaa, yakiwa mazingira kama yale yaliyosogeza chaguzi DRC.

Licha ya umuhimu wa kuchukua hatua hiyo, yaani uamuzi mgumu wa kuahirisha, ambao iwapo sababu zina nia njema ndani yake bila ushawishi wowote wa kisiasa, unaendana na msemo wa bora lawama ya kusogeza uchaguzi kuliko fedheha, ambayo wangeipata iwapo uchaguzi ungefanyika huku mambo yakiwa ovyo vituoni.

Lakini pamoja na hilo, kuahirishwa hata kama kulikuwa na sababu za msingi, kunaashiria uzembe wa hali ya juu ndani ya tume hizo zote za DRC na Nigeria.

Ni kwa vile zilikuwa na muda wa kutosha kuweka mambo sawa na kuhakikisha uwezekano wa vihatarishi vyovyote vya kuahirisha vinadhibitiwa.

Kusogeza chaguzi kwa wiki moja tu kunaashiria uzembe huo; huo ni muda mchache mno, ambao matatizo yaliyokwamisha kufanyika kama ulivyopangwa yangeweza kuzibwa au tahadhari zote kuchukuliwa kuhakikisha hayatokei na kusababisha ahirisho hilo.

Kwamba muda huo hauwezi kulinganishwa na miaka minne ya maandalizi na hivyo changamoto zilizoshughulikiwa kipindi hicho zingeweza kutatuliwa ndani ya kipindi hicho kirefu huku wakiwa wamepatiwa bajeti ya dola milioni 544.

Wengi wa Wanigeria ikiwamo vyama vya siasa na wanasiasa walilaani uamuzi wa INEC na kumkosoa vikali Yakubu kwa ahirisho hilo lenye maumivu na gharama kubwa kwao.

Kwa upande wake INEC haikufichua mara moja gharama za kifedha za kuahirisha, ingawa wachambuzi wanasema zinafikisha bajeti karibu na dola bilioni moja.

Lakini kwa raia wa kawaida, athari za kusogezwa kwa wiki moja zinaumiza na katika kesi nyingine zina gharama kubwa mno kwao.

Kwa vile Wanigeria hupiga kura tu katika vituo, ambavyo walijiandikisha tu, chaguzi nchini humo kwa kawaida huhusisha mipango makini mno na ghali ya safari.

Watu ambao wamehama makazi, wamebadili ajira au kuondoka nchini humo hulazimika kurudi katika vituo walivyokuwa wamejiandikisha kupiga kura huko nyuma.

Kwa maana kwamba wengi hulazimika wanapowasili kuishi katika nyumba za wageni ama hoteli kama si kujishikiza kwa marafiki au ndugu kutokana na kutokuwa na makazi katika maeneo hayo waliyoyahama.

Tayari kuna ripoti ya Wanigeria wengi waliopanda ndege kutoka Ulaya, Asia na Marekani, ambao mipango yao hiyo imevurugika vibaya na kuwaacha njia panda iwapo waingie gharama nyingine au waachane na habari za kupiga kura.

Ndani ya nchi kusafiri kwenda majimbo na maeneo mengine kupiga kura kumekuwa suala la kawaida nchini humo.

Kwa sababu hiyo watu wengi watakwama katika maeneo mengi mbalimbali na watabakia machaguo matatu;

Kurudi nyumbani na kisha kurudi tena vituo vya uchaguzi, kitu kitagharimu fedha za ziada; kuongeza mkao wao katika maeneo hayo ya kupiga kura kwa wiki moja zaidi kitu ambacho ni gharama za ziada au;

Kuamua kurudi nyumbani na kuamua kuachana na habari ya upigaji wa kura, kitu ambacho ni kujinyima wenyewe haki yao ya msingi na kidemokrasia.

Shule pia zilikuwa tangu mwanzo zimejipanga kwa kuzingatia ratiba ya awali ya INEC, ambayo pamoja na mambo mengine ziliruhusu wanafunzi kurudi walikojiandikisha kupiga kura, kupanga tarehe za mitihani na mengineyo.

Uchumi unaoyumba wa Nigeria pia umeathirika kutokana na biashara kulazimika kwa mara nyingine kufungwa ili kupisha uchaguzi baada ya awali kufanya hivyo wiki iliyopita.

Aidha kuahirisha uchaguzi kutaathiri mwitikio wa wapiga kura miongoni mwa Wanigeria milioni 84 waliojiandikisha kwa tukio hilo kwa namna nyingi.

Katika wiki moja hiyo kuna uwezekano wa wapiga kura wengi kutoweza kupiga kura au kutokuwa tayari kusafiri tena kwenda kupiga kura mbali na wanapoishi kwa sasa.

Hilo ni tatizo kwa taifa ambalo hivi karibuni limekuwa likihaha na mwitikio mdogo wa wapiga kura kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2015.

Baada ya kuuchelewesha kwa wiki sita, ni asilimia 33.5 tu ya waliojiandikisha kupiga kura walijitokeza katika uchaguzi huo.

Ndiyo maana tangazo la INEC la kuahirisha uchaguzi huo lilikumbana na hasira, ghadhabu na hali ya kukata tamaa miongoni mwa Wanigeria wengi.

Wengi wanailaumu kwa hatua hiyo kufanyika saa chache kabla ya uchaguzi, wanaona ingekuwa bora taarifa ingepatikana mapema ili waweze kurekebisha mipango yao na kuepuka kuingia gharama za kisaikolojia na kifedha bila msingi wowote.

Na zaidi wanauchukulia, uamuzi huo wa ghafla wa INEC kama dharau kwao na usiozingatia athari zitakazowapata raia.

Licha ya tangazo hilo kukiri ‘uamuzi mgumu’ kitu ambacho ni kweli kutokana na athari zake kwa raia, taifa na heshima yake (Tume) kitaifa na kimataifa kwa ujumla, hakukuwa na taarifa ya kuomba radhi kwa hatua hiyo inayotokana na uzembe wao wenyewe au kukiri athari za kufanya hivyo zitakazowakumba raia hasa baada ya awali INEC kudai kwa msisitizo mkubwa hakuna uwezekano wa kuahirisha saa 12 kabla ya tangazo lake lililodhihirisha ukinyonga!.

Kiukweli, uamuzi wa INEC ulihatarisha maisha ya maelfu ya vijana wa Nigeria. Kote nchini Nigeria vijana hawa waliachwa bila kulindwa, bila usalama katika vituo vya kura.

Aidha kuna waangalizi wa kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, ECOWAS, Umoja wa Ulaya pamoja na Taasisi za kimataifa za Marekani, International Republican Institute (IRI) na National Democratic Institute (NDI) zilizokuwa zimejiandaa kwa jukumu hilo siku hiyo.

Katika taarifa yao ya pamoja taasisi hizo zilisema wakati INEC ikiwa imepiga mahesabu vibaya juu ya changamoto zinazohusiana na usimamizi wa chaguzi, lakini pia ilikuwa bora zaidi kusogeza uchaguzi kuliko uwezekano wa kura kuvurugika siku ya uchaguzi kwa matatizo ya kilojistiki.

Lakini kuna uwezekano wa kuwa na waangalizi wachache wakati utakapofanyika Jumamosi hii kutokana na tarehe mpya kutokuwa katika mipango yao, hali inayoweza kuathiri uhalali wa uchaguzi huo.

Aidha bila shaka vyama vyote vya siasa ambavyo vina wagombea wanaoshiriki chaguzi vina uwezekano wa kuathirika na ahirisho hilo.

Vyama hivyo, bila kujali nguvu yao ya kisiasa vilimimina maelfu ya mawakala wa uchaguzi sehemu kadhaa za nchi kusimamia mchakato huo.

Na hivyo ni gharama kubwa kwao kurudia zoezi hilo. Ni tofauti na INEC, ambayo imehakikishiwa bajeti ya ziada na Hazina ya Taifa, wakati vyama vya siasa vikilazimika kutafuta rasilimali nyingine ili kuwapanga mawakala wao.

Iwapo INEC ingetangaza mapema angalau siku mbili au tatu lakini zaidi wiki moja kabla, waangalizi wa uchaguzi pamoja na vyama hivyo visingeingia gharama za kupeleka mawakala au waangalizi wao vituoni.

Matukio mengine yaliyokuwa yamepangwa kufanyika katika tarehe mpya za uchaguzi ni pamoja na harusi, mazishi, sherehe za uzinduzi fulani na mengineyo vimeathirika.

Baadhi ya matukio haya yaliyopangwa yalikuwa yamesogezwa ili kutogongana na tarehe za awali za chaguzi.

Aidha makundi mbalimbali mengine ikiwamo vyombo vya usalama vimeathirika bila kusahau INEC yenyewe ambayo licha ya kutokuwa na wasiwasi na bajeti kwa mgongo wa walipa kodi, taswira yake imeharibika vibaya ndani na nje ya Nigeria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles