26.9 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto alia na rushwa kwenye uchaguzi

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

NA GRACE SHITUNDU

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika vyama vya siasa nchini wamekuwa wakivunja sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Alisema hatua ya kushindwa kuwasilisha ripoti ya matumizi ya fedha za uchaguzi kwa wagombea wa ubunge, urais na udiwani inakwenda kinyume na sheria.

Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akizungumzia ripoti ya utafiti wa rushwa nchini, uliofanywa na taasisi ya Twaweza, ambapo ilibainika moja ya maeneo yaliyokithiri kwa rushwa ni sekta ya siasa.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, alisema mfumo wa sasa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), umekuwa na matatizo, ikiwemo ucheleweshaji wa kesi za rushwa pindi zinapofikishwa mahakamani.

Alisema kwa namna hali ilivyo sasa, ni lazima TAKUKURU wajitegemee na kuwa na mamlaka kamili ya kusimamia kesi hizo kuliko kusubiri uamuzi wa Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP).

“Kwa mfano jimbo langu mimi, Jimbo la Kigoma Kaskazini na baadhi ya majimbo mengine ya jirani katika Mkoa wa Kigoma, hautakiwi kutumia zaidi ya shilingi milioni 50 kwenye kampeni na sheria ipo wazi kabisa, na unatakiwa utoe ripoti ya jambo kama hilo.

“Tatizo ni kwamba ni ile ‘enforcement’ ya sheria inavyokuja, tangu mwaka 2010 mpaka sasa hakuna ukaguzi uliofanyika ili kujua kama kuna wagombea wametekeleza sheria hii kuanzia kwa mbunge hadi kwa rais,” alisema.

Alisema hatua ya kutofanyika kwa ukaguzi kama sheria ya matumizi inavyotaka, ni uthibitisho tosha kuwa rushwa bado ni tatizo nchini, hasa kwa wanasiasa.

“Tusipoondoa rushwa katika michakato ya uchaguzi, itakuwa ni ngumu kupambana nayo, kwa sababu mtu ambaye anaingia madarakani kwa fedha ya rushwa, akifika ni lazima atafute fedha kwa ajili ya kulipa,” alisema.

Zitto alisema wananchi wanaonyesha kukata tamaa na mapambano dhidi ya rushwa kwani asilimia 51 walisema rushwa haiwezi kuondolewa wala kupungua, asilimia 37 inaweza kupungua kidogo, lakini asilimia 70 wanaamini hata chama kingine kikija kutawala badala ya hiki kilichopo, hakitaweza kupambana nayo.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, wametoa mapendekezo ambayo yanaelekeza kuipa nguvu TAKUKURU, ya wao wenyewe kushitaki na kuendesha mashitaka bila kupitia kwa DPP.

Ripoti ya Twaweza iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam juzi, imeonyesha wananchi asilimia 89 wamewataja polisi kuongoza kwa rushwa wakifuatiwa na wanasiasa asilimia 85, afya 82, sekta ya kodi 80, ardhi 79 na sekta ya elimu 55.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles