32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

ZIJUE DILI ZILIZOJIFICHA ZENYE PESA NDEFU

Na ATHUMANI MOHAMED

BILA kuumiza kichwa sawasawa mafanikio ni jambo gumu kulifikia. Kwa maisha ya sasa, lazima akili yako ifikirie zaidi na zaidi ili kuweza kuyasogelea mafanikio.

Lipo tatizo moja kuu ambalo nimelizungumzia mara nyingi; hata wataalamu wengi wa mambo ya ujasiriamali na mafanikio wamekuwa wakisema jambo hilo. Namna tulivyoandaliwa na maisha.

Ukifuatilia wafanyabiashara wengi, wamerithi kwa wazazi wao, wachache waliibuliwa na ujasiriamali kutokana na maisha magumu nk. Waliobaki ambao kimsingi ni wengi, tumejengwa kwenye misingi ya kusoma, kupata kazi na kupokea mshahara.

Ndugu zangu, ajira siyo mstari mbaya, lakini kwa hakika kuwa mwajiriwa maana yake ni kwamba umeridhika na maisha ya kawaida. Kula, kuvaa, kusomesha watoto, kwenda likizo na kusubiri kustaafu.

Ndiyo ukweli ambao wengi wanaweza kuukimbia. Wachache sana kati ya wengi walioajiriwa, ambao ni mabosi maofisini na wenye vipato vya kuanzia angalau milioni tatu kwa mwezi ndiyo ambao wanaweza kupanga kidogo maisha yao (kama wana fikra za kijasiriamali).

Nimesema hivyo nikimaanisha kuwa unaweza kuwa mfanyakazi lakini mwenye fikra za kijasiriamali. Wale wenye kuishi kwa kujua kesho zipo, watazipata hawawezi kuwa na malengo na maisha yao ya baadaye.

Sasa basi, yawezekana umeajiriwa lakini unapaswa kushughulisha ubongo wako ili uwe na chako. Hata kama ni biashara ndogondogo, ukiwa nazo nyingi, kuna kitu utaingiza. Hata kama kesho bosi wako akikusimamisha kazi, hutapaniki, zaidi utaulizia mafao yako, utaendelea na biashara zako. Iko hivyo.

Kwa wale ambao si waajiriwa. Wapowapo tu. Hawa ni wale ambao ukiwauliza kuhusu maisha, watakujibu: “Hakuna kazi ndugu yangu, nimehangaika sana kutafuta kazi, hakuna.” Au mwingine atakuambia: “Ajira tatizo, biashara pia ndiyo balaa. Nawezaje kufanya biashara bila mtaji?”

Watu wa aina hiyo wapo wengi zaidi. Ajira, mtaji. Wenye ajira watakuambia, mshahara hautoshi. Hakuna kwenye afadhali.

Lakini je, umewahi kugundua kwamba, kazi unayoomba kila siku na unakosa, unaweza kuifanya peke yako kwa mtindo wa private au mobile (popote) na ukalipwa fedha nyingi zaidi?

Je, unajua kuwa, kazi unayofanya na kusubiri mshahara mwisho wa mwezi, unaweza kuifanya kwa mtindo huo bila kuathiri utendaji kazi wa mwajiri wako na ukapata pesa ndefu?

Katika mada hii nimekuandalia dili chache kati ya nyingi ambazo unaweza kuzifanya kwa kumfuata mteja na ukapata fedha nyingi.

GHARAMA ZA MATANGAZO

Kwanza kabisa nianze kwa kufafanua hili. Watanzania wengi hupenda visingizio, najua nikianza kutoa hizo dili, swali kuu litakuwa; je, vipi gharama za matangazo? Nami nakuuliza, si unamiliki simu?

Si una ukurasa wa Facebook, Instagram nk? sasa basi, social media zitakuwa mtangazaji wako wa kwanza na mkuu katika dili nitakazokupata hapa chini. Lakini hata redio mbalimbali nchini, ukiwa mdau wao ni rahisi kujitangaza.

Kazi yako ukipiga simu, unataja biashara yako na kuchangia mada au mazungumzo, mwisho unawaalika wadau kwenye biashara yako. Mara moja unakuwa umeshajitangaza na kujulikana na wadau wengi.

MOBILE BARBER SHOP

Nimetumia jina maarufu, lakini najua wengi mnafahamu kuwa namaanisha saluni ya kiume. Biashara ya saluni ya kiume ni kubwa na imepanuka. Ni biashara ya uhakika kwa sababu kati ya mambo muhimu mjini watu wanayozingatia ni usmart.

Kama wewe ni kinyozi hili ni dili zuri kwako. Siyo kila mtu ana muda. Wengine wana fedha lakini hawana muda. Kuna watu wanapenda kunyoa nywele, ndevu na huduma nyingine za saluni kama kufanya steaming, waves, black, facial, scub nk kila wiki lakini hawana muda wa kwenda saluni.

Changamkia hii dili. Kazi yako ni kununua mashine zako mbili na vifaa vingine vya kawaida, kisha unapachika jina mathalani JULIUS MOBILE BARBER SHOP. Utapiga pesa nzuri sana.

Kumbuka kwa sababu ni huduma ya kumfuata mtu kwake, bei haitakuwa ileile. Kwa wastani (kwa aina ya watu ninaowazungumzia hapa) bei ya kunyoa saluni ni wastani wa Tsh. 5000 (nywele na ndevu) kwa saluni nyingi za mijini.

Hapo bado scub, waves na huduma nyingine kama atapenda ambazo kwa watani mteja mmoja hugharamia si chini ya Tsh. 10,000. Ukimfuata kwake, itakuwa mara mbili au tatu na pengine ukalipwa zaidi kulingana na utakavyotoa huduma.

Kuna wagonjwa, wazee na watoto ambao ndugu zao hawataki usumbufu wa kuwapeleka saluni. Kuwa mjanja kwa kuchungulia hii fursa.

Nitakupa dili zaidi wiki ijayo. Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles