25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

ZIFAHAMU MBINU ZA KUUSHINDA MSONGO WA MAWAZO

Na Dk. Chris Mauki

Wakati kila mmoja wetu akijitahidi kusukumana na kukimbizana na maisha ya kila siku, jitihada hizi zinaambatana na misukumo na misongamano mbalimbali ambayo pasipo kukwepa inatuletea msongo wa mawazo “stress” na hii huweza kusababisha athari katika afya zetu na hisia zetu.

Ni muhimu sana kila mmoja wetu akafahamu namna au mbinu za kuushinda msongo huu wa mawazo kabla haujakuzidi na kuleta athari mbaya zaidi katika maisha yako. Labda kabla sijaendelea mbali ni bora ukafahamu kwa ufupi nini madhara ya msongo wa mawazo ili uweze kuuepuka. Nimeandika makala nzima ya kuhusu athari hizi kwa undani, waweza kusoma kupitia kitabu changu cha kwanza “Jitambue Kisaikolojia” au kwa kuingia kwenye tovuti yangu www.chrismauki.com.

ATHARI ZA MSONGO WA MAWAZO

Miili yetu imeumbwa kukutana na misongo ya mawazo na kukabiliana nayo, ingawa kiwango kidogo cha msongo wa mawazo hutusaidia kuepukana na baadhi ya hatari na kutufanya tuwe makini zaidi, kiwango hiki kinapozidi hutuletea madhara makubwa kiafya na kihisia pia. Dalili za madhara haya ni kama vile maumivu ya mara kwa mara ya kichwa, matatizo katika usagwaji wa chakula “digestive problems”, maumivu ya kifua, matatizo ya kukosa usingizi, na kuyumba kwa shinikizo la damu. Wataalamu wa afya wameeleza pia kwamba kuongezeka kwa msongo wa mawazo kunaweza kuongeza kiwango na mateso kwenye baadhi ya magonjwa aliyonayo mhusika. Matatizo kama vile shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, pumu, kisukari, sonona, magonjwa yanayohusiana na hofu, matatizo yanayohusiana na hisia, pamoja na matatizo au magonjwa ya ngozi huweza kuzidishwa kama mgonjwa anakiwango kikubwa cha msongo wa mawazo. Kwa kuongezea hapo, mwili kupunguza kinga, kuzeeka katika umri mdogo, na matatizo ya kupoteza kumbukumbu ni mojawapo ya athari za msongo wa mawazo.

Kwasababu ya kusumbuliwa na msongo wa mawazo wako wengine hujitumbukiza kwenye ulevi wa pombe, uvutaji mkubwa wa sigara, na dawa za kulevya lakini jitihada zote hizi za kupunguza “stress” huwa na athari mbaya zaidi kiafya. Hapa najaribu kukusaidia kuziona njia bora na rahisi za kukabiliana na msongo wa mawazo kiufanisi na ukizingatia kuiboresha afya yako.

MAMBO YA KUZINGATIA

Jifunze kusema hapana

Kwa kuamua kukubali kufanya kila kitu kinachokujia mbele yako, kukubali kila mwaliko ulio mbele yako, kukubali kuongea na kila mtu anayetaka kukuona au kukutana na wewe au pia kuamua kufanya vitu tele visivyoongeza thamani kwako kunaweza kukufanya uhisi kuchoka, kuzidiwa na kuwa mwenye msongo wa mawazo. Ukweli ni kwamba watu wenye ufanisi, watu wenye furaha na watu wenye maisha yenye uwiano katika yale wanayoyafanya hujizuia sana kuhusiana na muda wao na hujiwekea mipaka katika maisha yao, kwahiyo kujifunza kusema hapana kutakusaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuweza kuishi kwa ufanisi mkubwa katika maisha yako binafsi ya kila siku. Jaribu kufahamu madhaifu yako au yale usiyoyaweza, jifunze kujiwekea vipaumbele, jifahamu na jitambue, kuwa mwenye msimamo katika unachokitaka na usichokitaka na jiruhusu kuweza kusema “hapana” katika baadhi ya mambo. Hakika mwili na nafsi yako vitakushukuru sana kwa hilo.

Jaribu kuvuta pumzi kwa kina

Mara nyingi mtu anapokuwa na msongo wa mawazo hupumua haraka haraka na kwa pumzi fupi kwa ajili ya vile mwili wake unavyokabiliana na msongo huo “fight or flight response”. Hali hii inaweza kusumbua uwiano wa gesi ya mwili na kuongeza vipindi vya hofu na mshtuko, lakini hata hivyo kwa kupumua pumzi kubwa, ndefu na ya kina “breathing deeply” kunaweza kuwezesha mwili wako kupoa, kwasababu mtu anapopoa, na kuondokana na hofu kule kupumua haraka haraka hutulia.  Kwa kuamua kutumia mbinu hii ya kupumua pumzi ndefu na ya kina unaweza kuituliza mishipa yako na kuusaidia mwili wako kukabiliana na msongo wa mawazo. Jaribu kukaa katika mkao mzuri, nyanyua mabega yako ili kupanua kifua chako, weka mkono wako mmoja katika kifua chako na mwingine kwenye tumbo. Kwa kufanya hivyo utaweza kuona jinsi maeneo haya yanavyo ingia ndani na kutoka nje jinsi unavyo pumua. Wakati unapumua, vuta pumzi ndefu na kuitoa taratibu kutumia pua zako na uruhusu lile shinikizo la mawazo ya msongo kutoka kila unapotoa pumzi nje. Taratibu utaona kifua na tumbo lako vinapoa na kuanza kutulia. Baada ya kuiona tofauti katika kufanya haya basi endelea kuifurahia hali ya burudiko la nafsi mwili na moyo kwa muda kama wa dakika 10 au 20 kabla haujaendelea na mambo mengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles