SOCHI, URUSI
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin na mwenzake wa Jamhuri ya Czech, Milos Zeman, wanatarajia kukutana wiki ijayo nchini hapa.
Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Urusi, Aide Yuri Ushakov, wawili hao watakutana Novemba 21, mwaka huu, katika mji wa Sochi, uliopo kando mwa bahari nyeusi, ambapo watajadiliana masuala mbalimbali ya uchumi na biashara.
“Siku ya Novemba 21 katika mji wa Sochi kutakuwapo na mkutano wa viongozi hao wawili ambao watajadiliana masuala mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya mataifa haya mawili,” alisema msemaji huyo.
Alisema Rais huyo wa Jamhuri ya Czech atawasili nchini hapa kwa ziara ya kikazi kuanzia Novemba 20 hadi 24 na Novemba 22 atakutana na Waziri Mkuu, Dmitry Medvedev.
Msemaji huyo alisema baada ya viongozi hao wawili kukutana, baadaye Rais Zeman atahutubia Mkutano Mkuu wa Ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili.
Ziara hii ya Rais Zeman nchini hapa itakuwa moja kati ya ziara zake za mwisho za kutembelea mataifa mbalimbali kutokana na kwamba kipindi chake cha utawala wa miaka mitano kinamalizika majira ya baridi yajayo.
Taifa hilo linatarajia kufanya uchaguzi Januari, mwakani, ambapo kiongozi huyo atakuwa akitafuta nafasi ya kuchaguliwa tena kipindi cha miaka mingine mitano.