27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yawakimbiza vibaya Waarabu

Untitled-2JUDITH PETER NA THERESIA GASPER, DAR

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Yanga wanakutana na miamba ya soka barani Afrika, Al Ahly kwenye hatua ya 16 bora, huku wakionekana kuwazidi katika idara ya ushambuliaji kutokana na wingi wa mabao Wanajangwani hao waliyonayo.

Kwa kulinganisha viwango vya soka vya timu hizo, Al Ahly wamewazidi kwa mbali Yanga kutokana na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara nane huku Yanga wakiwa hawana historia ya kunyakua taji hilo.

Yanga wamefanikiwa kuingia raundi ya pili ya Klabu Bingwa Afrika kwa kuiondosha nje ya michuano hiyo, APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikiwa ni ushindi wa 2-1 ugenini na sare ya 1-1 nyumbani.

Katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamecheza michezo 21 sawa na Al Ahly kwenye ligi ya nchini Misri, lakini Wanajangwani hao wanaonekana kuwazidi wapinzani wao kwa kufanya vizuri zaidi.

Katika mechi 21 ambazo Yanga wamecheza Ligi Kuu, wamejikusanyia pointi 50 baada ya kushinda mechi 15, kufungwa moja na kupata sare mara tano, tofauti na miamba hiyo ya soka barani Afrika iliyofikisha pointi 47.

Al Ahly ambao wanaongoza Ligi Kuu ya nchini Misri kutokana na pointi 47 walizonazo, wamefanikiwa kushinda mechi 14, kufungwa mara mbili na kupata sare mbili huku washambuliaji wake wakitikisa nyavu mara 35 na kuruhusu kufungwa mabao 14.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, lakini safu yake ya ushambuliaji inaonekana kuwa imara zaidi kutokana na kutikisa nyavu mara 51 na kukubali kufungwa mabao 11 kwenye ligi hiyo.

Rekodi za timu hizo katika Ligi Kuu, zinaonesha kuwa Yanga ndiyo timu pekee iliyoruhusu nyavu zake kutikisika mara chache kutokana na mabao 11 waliyofungwa, huku Al Ahly wakifungwa mabao 14 ambayo ni machache ukilinganisha na timu nyingine katika ligi ya Misri.

Kulingana na rekodi za ligi msimu huu, safu ya ushambuliaji ya Yanga inaonekana kuwa imara zaidi kwa kufunga mabao mengi, ambapo mshambuliaji wake, Amissi Tambwe, amefunga mabao 17 huku Donald Ngoma akitikisa nyavu mara 13.

Tambwe na Ngoma ndio wanaweza kuwa tishio zaidi kwa Al Ahly wakati wakijiandaa kukutana mwezi ujao, lakini kwa upande wa Wamisri hao wachezaji  wanaoweza kuwasumbua Yanga ni kiungo, Abdalla El Saidi na mshambuliaji, Malick Evouna, waliopo katika kinyang’anyiro cha ufungaji bora.

Kwa upande wao Azam ambao pia wametinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, watakutana na timu ngumu kutoka nchini Tunisia, Esperance ambao wameshiriki mara nyingi michuano hiyo na kupata mafanikio.

Juzi wanalambalamba hao walifanikiwa kuwatupa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho, Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3, ikiwa ni ushindi wa mabao 3-0 ugenini na 4-3 nyumbani.

Azam wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuvuna pointi 50 kutokana na michezo 21 waliyocheza, sawa na wapinzani wao Esperance waliojikusanyia pointi 50 baada ya kushuka dimbani mara 19.

Rekodi za timu hizo zinalingana hasa katika upande wa ufangaji, ambapo kila timu imetikisa nyavu mara 37, lakini Azam wakiwa wamefungwa mabao 13 na Esperance 15.

Juzi mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche, aliweza kuweka rekodi baada ya kuifungia timu yake ya Azam mabao matatu ‘hat trick’ katika mchezo wa marudiano dhidi ya Bidvest.

Kutokana na mafanikio waliyopata Yanga na Azam kwa kuingia hatua ya 16 bora ya michuano ya kimataifa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amezipa siri ya ushindi inayoweza kuzisaidia kutinga hatua inayofuata ya robo fainali.

Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Azam na Bidvest Wits uliochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Nape alizitaka timu hizo kutafuta mbinu mpya na kuweka mikakati thabiti ya kuwakabili wapinzani wao.

“Nazipongeza Yanga na Azam kwa kufanikiwa kuingia hatua ya 16 bora, lakini sasa wataenda kukutana na Waarabu ambao wapo vizuri kwenye  soka, hivyo wanahitaji kufanya mazoezi ya kutosha na kujituma zaidi,” alisema.

Alisema kadiri wanavyozidi kusonga mbele watakutana na timu kubwa zenye ushindani na uwezo wa hali ya juu, hivyo ni vyema wakaandaa mikakati itakayowawezesha kufanikiwa na kufika mbali zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles