32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YATAMBA KUING’OA SIMBA KILELENI

Na CLARA ALPHONCE-DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga, imetua mjini Bukoba, mkoani Kagera, kwa ndege ili kuwakabili wenyeji wao, Kagera Sugar, leo katika Uwanja wa Kaitaba, huku ikitamba kushinda na hivyo kuing’oa Simba kileleni mwa ligi hiyo.

Yanga, iliyopo nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tisa, itashuka dimbani kusaka pointi tatu ili kujiweka sawa katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo yenye timu 16.

Mashabiki wa timu hiyo kwa muda wamekuwa hawaridhishwi na mwenendo wa timu yao, tofauti na msimu uliopita na hali hiyo imesababisha kuanza kumnyooshea vidole Kocha Mkuu wao, Mzambia George Lwandamina.

Akizungumzia mchezo huo, Lwandamina alisema ni mchezo mgumu, lakini ni muhimu wao kushinda kutokana na mazoezi waliyofanya kuikabili Kagera Sugar.

Hata hivyo, Yanga itaendelea kuwakosa wachezaji wake, Donald Ngoma na Thaban Kamusoko katika mchezo huo kutoka na kuwa majeruhi.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, alisema wamejipanga kutumia uwanja wao wa nyumbani vizuri na wanatarajia kuanza kupata ushindi katika mchezo huo dhidi ya Yanga.

Aliwataka mashabiki wa timu hiyo wasife moyo kutokana na timu yao kutofanya vizuri katika michezo yake iliyopita na kwamba huo ni upepo mbaya waliopitia na anaamini watakaa vizuri na timu kupata ushindi.

Yanga itashuka dimbani kuwavaa wenyeji wao hao huku wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 6-2, walioupata kwenye Uwanja wa Kaitaba, msimu uliopita.

Mbali na Yanga na Kagera Sugar, pia kutakuwa na michezo mingine ya ligi hiyo leo, ambapo Ndanda FC watakuwa nyumbani kuikaribisha Majimaji ya Songea, Ruvu Shooting itaikaribisha Singida United katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, wakati Mwadui FC wataialika Azam FC katika Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, huku Njombe Mji ikimenyana na Lipuli FC katika Uwanja wa Sabasaba, mjini Njombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles