BEIJING, CHINA RAIS,
Xi Jinping wa China ameuambia mkutano mkuu wa chama chake cha Kikomunsti kuwa taifa hilo lina mustakabali mzuri kiuchumi, licha ya kukiri kukabiliwa na changamoto kubwa kwa sasa.
Akifungua mkutano huo unaofanyika mara moja kwa kila miaka mitano jana, Xi ametetea juhudi za nchi yake kujiimarisha kwenye Bahari ya Kusini inayogombaniwa na majirani zake. Aidha ametetea siasa ya nje ya taifa hilo la pili kwa nguvu za uchumi duniani, mradi wake wa miundombinu unaofahamika kama ‘Mkanda Mmoja, Barabara Moja’ ambao unalenga kuimarisha uhusiano kati ya China, Ulaya na Afrika.
Hata hivyo, hotuba hiyo muhimu kwa nafasi ya Xi kisiasa, haikueleza kwa undani juu ya matatizo ya ndani, yakiwemo kuongezeka kwa pengo la kipato, ukosefu wa ajira, elimu na huduma za afya, miongoni mwa wananchi wa kawaida. Xi anatazamiwa kuchaguliwa tena kuongoza chama chake kwa miaka mingine mitano ijayo.