QATAR, DOHA
KIUNGO wa zamani wa klabu ya Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania, Xavier Hernandez ‘Xavi’, amedai kuwa, Kevin De Bruyne, ni Lionel Messi wa klabu ya Manchester City.
Xavi amesema kocha wa Man City, Pep Guardiola, ana bahati ya kuwa na mchezaji kwenye kikosi chake ambaye ana vitu kama alivyonavyo nyota wa Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, Messi.
Huu ni msimu wa pili kwa kocha Guardiola ndani ya kikosi hicho, msimu wa kwanza hakufanikiwa kupata taji la Ligi Kuu, lakini msimu huu ana matumaini makubwa ya kuwa bingwa kutokana na ubora wa kikosi chake.
Kiungo wa klabu hiyo, De Bruyne, ambaye ni raia wa nchini Ubelgiji, anaifanya klabu hiyo kuwa bora katika safu ya kiungo na ushambuliaji kutokana na kazi anayoifanya, hivyo Xavi amedai kuwa Guardiola amepata kiasi fulani cha ‘DNA’ kutoka Barcelona.
“Kikosi cha Pep Guardiola kinashinda kwa kuwa kinacheza kama timu, lakini hali hiyo inatokana na wachezaji wake kupambana kwa kasi ya hali ya juu kwa ajili ya ushindi.
“Katika klabu ya Barcelona tulikuwa na Messi na timu hii ya Manchester City wanaye De Bruyne, mara nyingi mchezaji huyo anakuwa na mpira, akifanikiwa kuwa na mpira unaamini kuwa kuna kitu maalumu anataka kukifanya.
“Si kila mchezo wanaweza kushinda mabao 3-0 au 4-0, hasa katika michuano ya Ligi Kuu, lakini ukiwa na wachezaji wa aina ya De Bruyne, kuna uwezekano wa kufanya hivyo, David Silva, siku hizi anacheza kwenye kiwango cha hali ya juu, nadhani kuna kitu kikubwa anakipata kutoka kwa Guardiola,” alisema Xavi.
Mchezaji huyo aliongeza kwa kusema hawezi kushangaa kuona wachezaji wa Man City wakicheza mifumo ambayo ipo katika klabu ya Barcelona kwa kuwa kocha wa timu hiyo amefanya makubwa ndani ya kikosi hicho.
“Nilikuwa najua kwamba Guardiola lazima aambukize baadhi ya vitu kutoka klabu ya Barcelona na ndio maana Man City kwa sasa wanaonekana kuwa na DNA ya Barcelona, kocha huyo alifanya makubwa akiwa na klabu hiyo, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuendelea kufanya hivyo akiwa na Man City.
“Msimu uliopita watu walikuwa wanasema kocha huyo atatekwa na mifumo ya nchini England, lakini kwa sasa wanasema Man City wanacheza mifumo ya Barcelona kutoka nchini Hispania,” aliongeza Xavi.