NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR
HUKU Serikali ya awamu ya saba ya Dk. Ali Mohamed Shein, ikitangaza kupambana na kubana matumizi, kusaidia kampuni za wazawa zipate zipate kazi kampuni mbalimbali, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na Wizara ya Fedha na Mipango zimeingia lawamani baada ya kudaiwa kutoa miradi mingi kwa kampuni ya ujenzi ya CRJE ya nchini China.
Kampuni hiyo inadaiwa kufanya ujenzi chini ya kiwango na kwa bei kubwa ambapo baadhi ya majengo yameanza kuonyesha hitilafu katika kipindi kifupi.
Taarifa za ndani ya serikali Visiwani Zanzibar, zinaeleza kuwa tayari Baraza la Wawakilishi limeingilia kati na kulazimika kuunda Kamati Teule kuchunguza ujenzi wa majengo tisa ya sekondari yaliyojengwa chini ya viwango.
Kamati hiyo teule iko chini uenyekiti wa Hamza Hassan Juma ambaye ni Mwakilishi wa Kwamtipura (CCM), ambaye hata hivyo aliliambia gazeti hili jambo hilo bado linafanyiwa kazi.
Katika majengo hayo yanayochunguzwa manne yamejengwa na kampuni ya CRJE inayodaiwa kulindwa na kupata zabuni kwa kutumia mgongo wa vigogo mbalimbali wa Serikali ya Zanzibar.
Kampuni hiyo imepewa zabuni ya ujenzi wa maduka Michenzani ambayo itagharimu Sh bilioni 27 lakini mpaka sasa bado hawajasainia mkataba na serikali bhuku ikielezwa kuwa wakat wowote kuanzia sasa watakamilisha jambo hilo.
Zabuni nyingine ilipewa kampuni hiyo ni ukarabati wa maduka (Jumba la Treni) lililopo Darajani ambalo mwanzo ilikuwa shilingi bilioni 8 lakini mpaka linakamilika iligharimu shilingi bilioni 12.
Ujenzi mwingine ni wa mifereji ya maji yanayotuama Kiembe Samaki kwa gharama ya Sh bilioni 3.4, ujenzi wa jalala (dampo) jipya la Kibere ambalo ni Sh Bilioni 24, ujenzi wa mtaro wa maji Mwanakwerekwe Sh bilioni 24
Hatua hiyo imezua malalamiko ya upendeleo na rushwa kwa kampuni hiyo ambayo zabuni nyingine zilifanywa bila uwepo wa kampuni nyingine shindani.
Wakati malalamiko hayo yakionekana kushika kasi tayari kumekuwa na wasiwasi kuwa fedha za umma zinazotumiwa na ZSSF inawekeza kwenye maeneo kampuni hiyo
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZEACA), Mwanaidi Suleiman Ali, akizungumza na gazeti hili, alisema hana taarifa zozote kama mamlaka hiyo imeshiriki kufanya uchunguzi.
“Kwa sasa sina taarifa yoyote kama ZEACA, tumeshiriki kuchunguza suala hili na ikizingatiwa kuwa leo siyo siku ya kazi naomba nikaulize kesho (leo) kazini baada ya hapo nitakupigia simu na kukupa majibu sahihi,” alisema Mwanaidi.
Alifafanua zaidi kuwa sababu za kutokufahamu kuhusu suala hilo ni kutokana na kuwa kamati zinazoteuliwa na serikali hazipendi kuingiliwa na mamlaka nyingine katika chunguzi zao.
“Ndio sababu nakuomba nikaulizie kesho kazini kama kuna maofisa ambao wameingia kwenye kamati hiyo lakini pia kama kuna uchunguzi wowote ambao umeshafanywa na mamlaka yetu,” alisisitiza.
Alipotafutwa Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya ujenzi ya CRJE Zanzibar, alijulikana kwa jina moja la Luo, alisema anahitaji kujua ni majengo yapi yaliyojengwa chini ya kiwango ili aende akayakague kabla ya kutoa majibu.