Na Bakari Kimwanga, Dodoma
WINGU zito limeendelea kutanda kuhusu uchunguzi wa sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusema hajapokea taarifa yoyote ya uchunguzi wa Sh bilioni 200 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Alisema kama angekuwa ameipokea kamwe haoni sababu ya kukaa nayo kimya.
Alisema pindi akiipokea taarifa hiyo ataiwasilisha kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kama utaratibu unavyotakiwa.
Pinda alitoa kauli hiyo bungeni Dodoma jana, alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo baada ya kuulizwa swali na Mbunge wa Ole, Rajab Mbaruk Mohamed (CUF).
Mohamed alitaka kujua licha ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kusema amemkabidhi ripoti hiyo, ni sababu gani zinazochelewesha kupelekwa bungeni.
Waziri Mkuu, alisema alichokisema juzi bungeni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi ni sahihi kwani hadi sasa hajaipata ripoti hiyo.
“Mheshimiwa mwenyekiti, unajua tangu mwanzo alipouliza nilijua swali lile la mwanzo ilikuwa ni kutafuta namna ya kupenya kuingia kwenda kwenye jambo lenyewe.
“Labda niseme hivi, juzi nilimuona mheshimiwa Lukuvi akitoa maelezo hapa, ni maelezo ya kweli na hakuna sababu yoyote ya kuficha. Sijapokea ile taarifa kutoka kwa CAG, nataka na mimi nirudie kusema nitakapokuwa nimeipokea sina sababu yoyote ya kukaa nayo, nitamkabidhi Spika kama utaratibu unavyotaka basi,” alisema Pinda.
Akizungumzia uamuzi wa wafadhili kugoma kutoa fedha, alisema wamekuwa na sababu mbalimbali ikiwamo suala la kesi ya IPTL jambo ambalo limekuwa likiwaumiza Watanzania bila sababu.
“Wafadhili hawa tunaowaita kwa jina la heshima zaidi wahisani wa maendeleo, mara nyingine wanakuwa na sababu zao mbalimbali, hili la kesi limejitokeza safari hii, lakini utakumbuka karibu bajeti mbili zilizopita kumekuwa na malalamiko.
“Vilevile tulikuwa tunachelewa sana kupata misaada kutoka kwao, pengine mpaka miezi minne, wakati mwingine tunamaliza bajeti hayo wala hayakutekelezwa, sasa kwa hili ambalo limesemwa mahsusi ni kweli na mimi nimelipata nimelisoma na hao watu wanasema wanangoja waone taarifa ya CAG itolewe ibainishe yaliyomo katika taarifa hiyo na wao kama wataridhika ndipo wataweza kutoa hizo fedha.
“Mimi nasema in sha allah, nadhani yatabainika na matumaini yangu kwamba watatoa, jambo ambalo kidogo linanisononesha ni pale unapokuwa katika jambo ambalo uamuzi wake unaweza ukagusa watu watatu wanne, lakini unafanya uamuzi ambao unakwenda kuathiri jamii ya Watanzania wengi, hasa wale wa kijijini, kidogo inanisumbua sana kwa sababu nilidhani njia rahisi ni kuwachukulia hatua hao watakaoonekana kulingana na hiyo taarifa,” alisema Pinda.
Alisema pamoja na hilo, lakini ingekuwa vema kwa watakaokuwa wamebainika wametenda mambo ambayo ni nje ya utaratibu wa nchi wazo la wahisani lingekuwa kwa Serikali kuwachukulia hatua kali.
Akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kuhusu changamoto fedha na kuathiri utekelezaji wa bajeti, Pinda alikiri hali hiyo na kusema kuwa kwa sasa wamekuwa wakichukua hatua kadhaa ili kukabiliana na hali hiyo
“Mara ya mwisho ni karibu Sh bilioni 13 hivi, tulichokubaliana tulipeleka maombi Wizara ya Fedha na tunajaribu kui-push (kusukuma) ili tuweze kupata hizo fedha maana na kubwa tulisema kwamba tulilazimika kidogo kuongeza idadi kidogo ya wanafunzi baada ya kufanya uamuzi wa kuongeza wale wanafunzi ambao wapo kwenye fani ya Sayansi,” alisema.
Kafulila na IPTL
Baada ya maswali na majibu, wabunge walichangia mpango wa maendeleo ya taifa ya mwaka 2015/16 ambapo Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema anashangazwa na Serikali kuendelea kukalia taarifa ya uchunguzi hali ya kuwa imeshakabidhiwa kwa Serikali kwa mamlaka husika.
“Tunataka taarifa iletwe hapa na hatuwezi kuruhusu familia ya watu watano waendelee kutumia fedha za walipakodi huku wananchi wanaendelea ‘kusafa’, hili hatukubali ni lazima ripoti hii iletwe hapa,” alisema Kafulila.
NAIBU WAZIRI KUTOLEWA KAFARA
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema), alisema kutokana na ripoti hiyo ya IPTL, hivi sasa kuna mpango wa kumtoa kafara naibu waziri mmoja ndani ya Bunge.
Alisema kutokana na hali hiyo katu hawatokubali kwa ripoti hiyo kumuhusisha mtu mmoja badala ya watu wote waliofanya makosa.
“Kuna taarifa naibu waziri mmoja anataka kutolewa kafara hapa, kwa hili tunapenda kuwaambia hatukubali… hatukubali, tutang’oa na bati lenyewe…lazima ripoti yote iletwe kama ilivyokuwa kuliko mkaichakachua na kutaka kumtoa kafara mtu mmoja kwa lengo la kuwalinda watu wengine, hili hapana,” alisema Wenje.