24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wenye kangoba wafunguliwa milango kuuza korosho

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amesema amewasamehe walionunua korosho kwa mfumo wa kangomba huku akiagiza Sh bilioni 50 zipelekwe kwa ajili ya kulipia wakulima 18,103 wenye kilo zaidi ya 1,500 za korosho.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo mkoani Mtwara jana akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani humo.

Alisema ameamua kuwasamehe watakaokiri kuwa walikuwa kangomba lakini wasirudie kosa hilo katika msimu ujao kwa sababu wanaoumia ni wakulima wa chini.

“Watakaokiri kuwa walikuwa kangomba na wamefanya hivyo kimakosa tuwaangalie kuwalipa kwa sababu ni wengi akiwamo mwenyekiti wangu wa CCM wa mkoa.

“Kufanya kosa si kosa lakini kurudia kosa ndiyo kosa, wakiri kwanza kuwa nilinunua kilo kadhaa kwa fulani… wa namna hiyo walipeni.

“Lakini wasirudie kwenye msimu unaokuja, kangomba imekuwa biashara ya kila mmoja sasa nimewasamehe lakini waandike kwamba mimi nina kagomba kangu kilo fulani mwaka huu ni wa neema,”alisema Rais Magufuli.

Alisema kwenye uhakiki wa wakulima waliokuwa na kilo zaidi ya 1,500, walikuwa 18, 103 hawajalipwa, waliolipwa ni wachache na uchambuzi wake umekamilika isingekuwa rahisi kutoa fedha bila uchambuzi.

“Kati ya majina hayo yamepatikana majina 780 hawana mashamba wala hawana mkorosho lakini walikuwa wanadai nao wana kilo zaidi ya 1,500…sasa ziletwe Sh bilioni 50 kuanzia kesho (leo) au kesho kutwa (kesho) zikiisha zinaletwa nyingine.

Vilevile alisema wapo wakulima wa korosho waliolipwa na walikuwa na madeni, lakini anapokuja mwenye deni anasema hajalipwa korosho, hivyo kila mmoja anasema ni korosho.

“Kuna mtu mmoja amekaa siku 20 hotelini hapa Mtwara hajalipa alipotakiwa kulipa akasema hajalipwa korosho, naona polisi wamemshikilia wanashughulika naye.

“Ninayo orodha ya waliolipwa, nitamwachia Mkuu wa Mkoa ili akashirikiane na wakuu wa wilaya, RC kawaumbue wote wanaosema hawajalipwa na kwenye orodha ile wapo, akisema hivyo mshike muweke ndani,”aliagiza Rais Magufuli.

Akizungumzia kuhusu Uwanja wa Ndege wa Mtwara, Rais Magufuli alisema Serikali imeamua kufanya upanuzi wa uwanja huo kutokana na uchakavu wa miundombinu kwa kuwa ulijengwa wakati wa ukoloni mwaka 1952 hadi mwaka 1953.

Alisema haiwezekani kutumia miundombinu ya miaka hiyo kwa wakati wa sasa, hivyo wanajenga kuiweka ya kisasa na kwamba utaongezwa urefu wa kurukia, upana kutoka mita 30 hadi mita 45 na utawekwa taa ili usiku, mchana mvua zinaponyesha uweze kutumika.

Rais Magufuli alisema mradi huo utakapokamilika mwaka 2020, uwanja utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa na ndogo na utafanya kazi mchana na usiku.

Alisema kupanuliwa kwa uwanja huo, mkoa huo pia utapata fursa nyingi za uwekezaji ikiwamo viwanda, gesi, makaa ya mawe na utalii.

“Ndugu zangu tumeamua kupanua uwanja huu lengo likiwa ni kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya nane na sita tayari zimewasili. Lengo letu tunataka ndege hizi zifike maeneo mengi ya nchi yetu.

“Ndiyo maana pia tunafanya upanuzi kwa viwanja 11, ikiwamo Iringa, Ruvuma, Mara, Shinyanga, Iringa, Rukwa, Kigoma,”alisema.

Alisema upanuzi huo umeanza Juni mwaka jana na utakamilika Septemba mwakani kwa gharama ya Sh bilioni 50.4 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Alisema ameuona muda aliopewa kandarasi wa kufanya uhamasishaji na alitakiwa awe amemaliza lakini anaidai Serikali asilimia 10 na baadaye asilimia 15 ili akamilishe hilo.

“Nimemwuliza waziri (Isack Kamwelwe) ameshazungumza na mwenzake Waziri wa Fedha, kulijadili hilo, amejibu hajafanya hivyo kwa mdomo, hilo nalo ni tatizo la mawaziri wangu kutowasiliana, wangefanya hivyo inawezekana ingekuwa imeshatolewa.

“Sasa naagiza ndani ya siku tano hizo fedha ziwe zimefika hapa kwa kandarasi. Nataka nimwambie mkandarasi kazi aliyofanya Mwanza haikuwa nzuri, nashangaa kwanini wamempa tena hapa, alisuasua sana, akawa anaomba malipo mengine ambayo hakuyafanyia kazi akishirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania.

“Utakapopata hizo fedha ambapo utapewa Sh bilioni saba ndani ya siku tano na ole wako usifanye kazi,”alisema.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli alimwagiza mkandarasi huyo kuwa atakapopewa hizo fedha ndani ya siku tano afanye kazi usiku na mchana.

“Mnapoomba kazi mfanye, hauwezi kuja hapa kufanya uhamasishaji unakuta malori mawili ambayo yametegeshwa kwa sababu wanajua ninakuja angalau niyakute, hata hili greda nimeliangalia tairi za mbele zimekwisha,”alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli aliwataka viongozi wa Mkoa wa Mtwara kuacha kugombana kwani kwa kufanya hivyo wawekezaji watashindwa kuwekeza katika eneo hilo.

“Viongozi mmekuwa mkilumbana mara kwa mara na mmekuwa na makundi yaani kila kiongozi ana kundi lake na mnapigana madongo, unakuta huyu haelewani na huyu.

 “Niwaombe ndugu zangu wa Mtwara, majungu hayaleti maendeleo, kama kuna mahali mjiombe au muombeane msamaha mnaleta na samaki mnamla…pataneni tunawacheleweshea wananchi maendeleo.

“Wakati mwingine mnachongeana wenyewe nashindwa hata niamue lipi, ukitaka huyu unakuta amepigwa dongo na wanaofanya hivyo ni wa Mtwara, hivyo wanawapa kazi ngumu na wenye kusikia na wasikie.

“Utakuta mwenyekiti wa zamani haelewani na wa sasa wa miaka hiyo haelewani na huyu, mbunge huyo haelewani na huyu, tuyamalize Mtwara tujenge taifa, tuna changamoto nyingi katika mkoa yanayohitaji maendeleo, mkoa huu Serikali yangu nimeamua kuubeba uwe wa mfano.

“Mtwara ya kweli haiwezi kupatana kama viongozi wanagombana, nimelisema hili kwa uwazi kama kuna lililowagusa liwashukie, wakalale nalo, wakagalegale nalo kwa manufaa ya Mtwara,”alisema Rais Magufuli.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alimshukuru Rais Magufuli kwa kununua korosho baada ya kuona hali ya soko inavyokwenda ikiwamo kudorora kwa minada na baadaye Serikali kununua korosho kwa Sh 3,300.

 “Baada ya malipo hayo lakini hayajakamilika kwa asilimia 100 na yapo manung’uniko kwa wananchi kutolipwa, nimewaagiza wakuu wa wilaya kupokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi.

 “Sh bilioni 10 zipo benki hazijakwenda kwenye akaunti kutokana na majina ya wakulima kutolingana na nyaraka zilizopo,”alisema.

Alisema viongozi wa vyama vya msingi wamekuwa wabadhirifu ambao wameorodhesha majina ya wakulima wa korosho wanaohitaji kulipwa huku korosho zikiwa hazijaonekana kwenye maghala na wananchi kubaki na karatasi zao.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuna korosho hazikuwa na ubora badala ya kurudishwa kwa wananchi walitafuta ghala wanalolijua wao na kumuuzia huyo mtunza ghala na wakarudi kwa wakulima kuwaambia kuwa Serikali imekataa korosho hizo.

Pia alisema wakulima 96 waligundulika kujihusisha na kangomba na baadhi yao kukiri kwa maandishi na wengine kushindwa kutoa maelezo ya kuthibitisha upatikanaji wa korosho zao.

“Mambo mengine yaliyogundulika mkulima hewa alikiri kupokea fedha Sh milioni 37 kutoka kwa raia wa Msumbiji anunue korosho Mtwara akilipwa anazirudisha Msumbiji kwa tajiri yake na alinunua kilo 41,287,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles