Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuendelea kupiga hatua kubwa katika kuboresha mawasiliano nchini.
Waziri Nape ametoa pongezi hizo Julai 8, jijini Dar es Salaam wakati wa jukwaa la TEHAMA lenye lengo la kuwakutanisha wadau wa Tehama kujadili changamoto mbalimbali za kujipatia ufumbuzi.
Amesema TTCL imewezesha wananchi kutumia Internet bure kwenye maonyesho kwa kufunga wifi katika maeneo 17 ndani ya viwanja hivyo ambapo mwananchi anapokuwa hapo anapata huduma ya internet bure.
“Nipende kuwapongeza sana TTCL kwa kuwezesha huduma ya mtandao bure kwenye haya maonyesho kwani tulipeleka mapendekezi yetu kwa kuchelewa sana lakini wameshughulikia na huduma inapatikana,” amesema Nape
Katika hatua nyingine, ametoa rai kwa waandaaji wa maonyesho hayo kujitahidi maonyesho yajayo yawe kidigitali ikiwa ni pamoja na kuweka anuani za makazi ili kurahisisha upatikanaji na urahisi wa maonyesho hayo.