Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameahidi kumsomesha Wakonta Kapunda (26) ambaye alipata ulemavu unaosababisha aandike kwa kutumia ulimi.
Wakonta ambaye ameishia kidato cha sita alipata ajali mwaka 2012 mkoani Tanga alipokuwa akienda katika sherehe za mahafali yake.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Dk. Reginald Mengi inayojihusisha na watu wenye ulemavu (DRMF), amesema atawasiliana na familia ya binti huyo ili kumwezesha kutimiza ndoto zake.
“Serikali inaheshimu na kulinda utu wa jamii mbalimbali wakiwamo watu wenye ulemavu, tutaendelea kusimamia ulinzi imara kwa watu wenye ulemavu na kuchukua hatua kali kwa yeyote atakaye wanyanyapaa na kuwaficha,” amesema Majaliwa.
Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara nchini kutenga sehemu ya faida wanazopata kusaidia watu wenye ulemavu kwa sababu suala la kuwahudumia watu wenye ulemavu si la Serikali pekee bali jamii nzima.
Amesema taasisi hiyo ni kielelezo muhimu cha mchango wa Dk. Mengi kwa watu wenye ulemavu hapa nchini na kuwataka watu wengine waige mfano huo.
Naye Dk. Mengi ameahidi kutoa Sh bilioni 5 kuwezesha ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya watu wenye ulemavu kitakachojengwa jijini Dar es Salaam.
“Usilalamike huna miguu au mikono bali tumia kikamilifu kile kilichobaki,” amesema Dk. Mengi.