Na ESTHER MBUSSI-DODOMA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameviagiza vyombo vya dola nchini kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bodi ya Sukari na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kudhibiti na kuziba mianya ya magendo katika uingizaji holela wa sukari na mafuta ya kula.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge hadi Novemba 6, mwaka huu.
Alisema hatua hiyo inatokana na mjadala uliojitokeza bungeni kuhusu suala la usimamizi katika uingizaji sukari na mafuta ya kula.
Alisema Serikali kwa upande wake inaimarisha taratibu za uingizaji wa sukari na mafuta ya kula kwa kuweka madaraja na usimamizi makini.
HALI YA CHAKULA
Akizungumzia hali ya chakula nchini, Waziri Mkuu alisema hali ya uzalishaji mazao ya chakula na upatikanaji wake imeendelea kuimarika, ambapo kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika Juni mwaka huu, inaonyesha uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2017/18 ni tani milioni 16.9.
“Kati ya hizo tani, milioni 9.5 ni mazao ya nafaka na tani milioni 7.4 ni mazao yasiyo ya nafaka, ambapo kutokana na uzalishaji huo na kwa kuzingatia mahitaji ya chakula nchini ambayo ni tani milioni 13.6, kutakuwa na ziada ya tani milioni 3.3.
“Hata hivyo, serikali inawasihi wananchi kutumia akiba hiyo ya chakula kwa uangalifu, kwani zipo nchi jirani ambazo zina uhaba mkubwa wa chakula,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu aliziagiza taasisi zote zinazosimamia elimu ya lishe na afya kuongeza nguvu zaidi ili kupunguza kiwango cha udumavu na utapiamlo, hususan kwa watoto.
ZAO LA KOROSHO
Waziri Mkuu alisema kuhusu zao la korosho, mfumo wa ununuzi kupitia vyama vya ushirika unapata mwitikio mzuri kutoka kwa wakulima na wanunuzi.
“Hali hiyo imesaidia wakulima kupata bei za ushindani ambapo kwa msimu wa 2017/18 ilifikia Sh 4,100 kwa kilo, ikilinganishwa na Sh 2,700 msimu wa 2016/17.
“Aidha, uzalishaji umeongezeka, ambapo jumla ya tani 296,281 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi takribani trilioni 1.12 zilikusanywa na kuuzwa kupitia vyama hivyo ikilinganishwa na tani 265,000 kwa msimu uliopita,” alisema.
ZAO LA CHIKICHI
Kuhusu chikichi alisema serikali imeweka mkakati wa kuimarisha zao hilo, ambapo alieleza mkakati huo una lengo la kuiwezesha nchi kuachana na uingizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
“Hivi sasa nchi inatumia takribani dola za Kimarekani milioni 294 kila mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta hayo, lakini mikakati iliyopo ni kuimarisha zao hilo na uanzishwaji wa kituo cha utafiti wa zao la chikichi katika eneo la Kihinga, mkoani Kigoma.
“Hatua nyingine ni kuandaa mpango mkakati wa uzalishaji wa miche bora ya chikichi milioni 20 ifikapo mwaka 2021, ambapo kwa kuanzia, mwaka 2018/19, serikali inakusudia miche bora milioni 10, kisha kusambazwa kwa wakulima.
“Hatua ya tatu ni kuandaa mpango mkakati wa miaka mitano wa utafiti wa mbegu bora ili kuongeza tija kutoka tani 1.6 hadi kufikia tani 4.0 za matunda ya chikichi kwa hekta kila mwaka,” alisema.
Waziri Majaliwa pia alieleza mikakati ya kuweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya uchakataji zao la chikichi.
Pamoja na mambo mengine, aliainisha mkakati huo kuwa ni kusimamia vituo vikuu vya uzalishaji vya Gereza la Kwitanga, Ilagala na JKT Bulombora na kutenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
Alisema serikali imeamua kurejesha ununuzi wa mazao makuu ya biashara kupitia vyama vya ushirika kwa lengo la kuwanufaisha wakulima.
Alifafanua kuwa, katika kufanikisha azma hiyo, serikali inasimamia matumizi ya mifumo mbalimbali ya masoko, ikiwamo stakabadhi ghalani na soko bidhaa.
“Matumizi ya mifumo hiyo yamechangia kuboresha ununuzi wa mazao hayo ambayo biashara ilikuwa ikifanyika kwa njia ya mnada na kusimamiwa na vyama vya ushirika, imeleta chachu ya ushindani, hivyo kumpatia tija mkulima,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa ambao hawajaanza kutekeleza kampeni ya kuhamasisha wananchi kupima Virusi Vya Ukimwi (VVU), aliyoianzisha Juni 19 mwaka huu, kuanza utekelezaji wake