Na MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa amepongeza ujenzi wa kiwanda cha Morris Philip Tanzania Ltd kinachojengwa mkoani Morogoro, huku akisema ujenzi huo ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Majaliwa alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki akiwa katika ziara mkoani humo, ambapo mbali na kupongeza ujenzi huo pia aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa bidii ili kuwavutia wawekezaji.
“Nitumie fursa hii kumpongeza mwekezaji wa kiwanda hiki cha Kampuni ya Philip Morris Tanzania Limited kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na rais wetu za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,” alisema Majaliwa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira kubwa kwa wananchi wake katika kupambana na suala zima la umasikini.
“Nimepata taarifa kuwa Kampuni ya Philip Morris imekuwa ndio inayoongoza kununua tumbaku inayolimwa hapa nchini. Lakini sasa wameamua kuja kuwekeza kwa kujenga kiwanda, hivyo inamaanisha ununuzi wa tumbaku utaongezeka.
“Hili ni jambo la kufurahisha kwani itaongeza kipato kwa wakulima wetu, kiwanda kikianza uzalishaji kitaanza kulipa kodi na hivyo kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Majaliwa.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, aliwaomba wakazi wa Mkoa wa Morogoro kujitokeza na kutumia fursa ya kiwanda hicho ili kupata ajira katika kiwanda hicho.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Philip Morris Tanzania Limited, Can Uslu, alisema kampuni yake imeamua kuwekeza hapa nchini baada ya kuridhishwa na utulivu uliopo.
Uslu alisema kiwanda hicho kitasaidia wananchi kupata ajira za moja kwa moja takribani 100 na zile ambazo si za moja kwa moja zaidi ya 2,000, huku akisisitiza kuwa bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa na viwango vya kimataifa.
Alisema kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Sh bilioni 60 kwenye ujenzi wa kiwanda hicho ambacho ujenzi wake ulianza mwaka 2015 na kinatazamiwa kuanza kufanya kazi ya uzalishaji wake mwezi ujao.