29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mhagama awaomba wadau kuboresha Taasisi za Wenye Ulemavu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ametoa wito kwa wadau mbali mbali wa maendeleo kusaidia kuboresha miundo mbinu katika vyuo vya ufundi vya watu wenye ulemavu ambavyo vipo katika kanda zote hapa nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akihutubia katika hafla ya kukabidhi mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation. Wengine ni Naibu Waziri wake (Watu wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga (wa pili kulia), Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof, Jamal Katundu (kushoto) na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa (wa kwanza kulia).

Ametoa wito huo jijini Dar es Salaam alipokuwa akipokea mabweni mawili katika chuo cha Ufundi Stadi kwa watu wenye ulemavu cha Yombo ambayo yamefanyiwa ukarabati na Shirika lisilo la kiserikali la Nyota Foundation kwa gharama ya Sh milioni 80.

“Sisi kama serikali tumejitahidi sana kuboresha vyuo hivi lakini niwaombe wadau wengine, makampuni, taasisi mbali mbali za kitaifa na kimataifa waviangalie sana vyuo vyetu. Vyuo hivi vinakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundo mbinu mbali mbali pamoja na upungufu wa miundombinu muhimu vikiwemo vyoo, madarasa, mabweni na miundombinu nyinginezo,” amesema Mhagama.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, kwa takwimu za mwaka 2019/2020, Tanzania ilikuwa na jumla ya watu 55.9 milioni; Kati ya idadi hiyo, watu milioni 2.5 ni wenye ulemavu na hivyo kuongeza mahitaji ya huduma na miundo mbinu mbali mbali kwa ajili ya kundi hilo.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, katika hafla ya kupokea mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo.

Awali, akimkaribisha Waziri Mhagama katika hafla hiyo, Naibu wake anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amempongeza Kiongozi huyo wa Wizara kwa kujitoa kwake katika kuboresha mazingira na hali za watu wenye ulemavu kupitia kuwashirikisha wadau mbali mbali wa maendeleo.

Mwakilishi wa Shirika la Nyota Foundation, Zainab Mvungi, ameishukuru serikali kwa kuruhusu ukarabati huo kufanyika pamoja na kutoa ushirikiano wakati wote walipokuwa wakifanya kazi hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwa ameongozana na wawakilishi wa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo wakati wa hafla ya kupokea mabweni ya chuo hicho yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo kinachomilikiwa na serikali kilianzishwa mwaka 1973. Chuo hicho ambacho ni kwa ajili ya Kanda ya Mashariki ni miongoni mwa vyuo sita (6) ambavyo vipo katika kanda mbali mbali hapa nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Vyuo vingine vipo Kanda ya Kusini (Mtwara), Magharibi (Tabora), Ziwa (Mwanza), Kaskazini (Tanga) na Kati (Singida).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles