*Awataka waache kutumia mabavu
*Akoshwa na Mkurugenzi wa MAUWASA
Na Samwel Mwanga, Maswa
WAZIRI Wa Maji, Jumaa Aweso amewaonya Wakurugenzi wa mabonde tisa ya maji nchini kuacha kutumia mabavu katika kulinda vyanzo vya maji kwani jamii haina shida katika kulinda vyanzo hivyo.
Pia amewataka maafisa wa mabonde hayo kuacha tabia ya kushinda ofisini na kuchezea kompyuta muda mrefu huku vyanzo vya maji vikiharibiwa kwa kufanyika shughuli za kilimo na shughuli za madini kwenye vyanzo hivyo.
Akizungumza Julai 29, 2022 kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Zanzui, Mwadila na Kitongoji cha Jashimba mjini Maswavya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aweso amesema jukumu la kulinda na kutunza vyanzo vya maji ni la kila mmoja hivyo ni vizuri watu wakashikamana.
Amesema haiwezekani kuona chanzo cha maji kimevamiwa na shughuli za kilimo zimefanyika na mazao yanapofikia hatua ya kuvunwa ndipo Afisa wa bonde anakuja kuyakata jambo hilo haliwezekani na hawezi kukaa katika Wizara ya Maji akiwa na Maafisa wa namna hiyo.
“Maafisa wa bonde tokeni ofisini nendeni huko kwenye mabonde mkatoe elimu kwa jamii jinsi ya kutunza vyanzo vya maji na siyo mnakwenda kufyeka mazao ya watu waliovamia maeneo ya chanzo wakati wanalima mlikuwa wapi?,” amesema Aweso.
Waziri Aweso amesema kuwa jamii ikielimishwa juu ya utunzaji wa chanzo cha maji haina shida huku akitolea mfano bwawa la New Sola maarufu bwawa la Zanzui linalomilikiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(MAUWASA) lilivyotunzwa na bonde la Ziwa Victoria na kuendelea kuwahudumia maji wananchi wa mji wa Maswa na vijiji 12.
“Ulindaji na utunzaji wa rasilimali za maji unaanza na mimi,unaanza na wewe,unaanza na sisi sote hivyo ni vizuri tushirikiane kwa pamoja kwa ajili ya manufaa yetu na manufaa ya vizazi vijavyo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(MAUWASA), Mhandisi Nandi Mathias kwa utendaji mzuri wa kazi.
Amesema kuwa ukimsikiliza Mhandisi Nandi utajua anaifahamu kazi yake hivyo kwa kutambua hilo kupitia maombi ya mamlaka hiyo ya kuomba fedha za miradi ya maji ameruhusu kutolewa.
“Hapa mna Mkurugenzi mzuri sana na ukimsikiliza unajua anaijua kazi yake hivyo namwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kutoa zaidi ya Sh milioni 350 ili usambazaji wa maji katika mji wa Maswa uendelee pia atoe Sh milioni 200 ili ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita za ujazo milioni mbili uanze kwenye kijiji cha Mwadila.
“Pia nakuagiza Mkurugenzi wa Mauwasa ujenge vituo vitano vya kuchotea maji katika kitongoji cha Jashimba kwani kipo kituo kimoja tu ambacho hakitoshelezi,”amesema.
Naye Mkurugenzi wa Raslimali za Maji wa Wizara ya Maji, Dk. George Lugomela amesema wanafanya ziara ya siku 30 na Waziri Aweso kwa ajili ya kutembelea na kuona jinsi vyanzo vya maji vinavyolindwa kupitia Mabonde tisa ya maji yaliyopo hapa nchini.