NA BENJAMIN MASESE- SHINYANGA
SERIKALI imewaonya wafanyakazi wa mizani nchini kuacha vitendo vya vitendo vya rushwa kuleta tija na ufanisi wa kazi zao katika usimamiaji na ulinzi wa barabara.
Imesema ikiwa watumishi hao watafanya kazi kwa weledi na uadilifu Serikali itaendelea kunufaika na miundombinu yake ya barabara na mizani ambayo imegharimu mabilioni ya fedha.
Onyo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sektaya Ujenzi), Elias Kwandikwa.
Alikuwa akikagua mzani wa Tinde na Mwendakulima ambako alikemea vitendo vya rushwa vinavyofanywa kati ya watumishi na madereva wa malori na basi za abiria.
Waziri aliwataka watumishi hao kufuata sheria na taratibu za kiutumishi na kuwaajibisha madereva wanaozidisha uzito na si kuomba rushwa.
Kwandikwa alisema kama wizara imepokea taarifa ya vitendo vinavyofanyika katika mizani mbalimbali na imeamua kupita kwa lengo la kuwaonya na kuwakumbusha kufuata sheria na taratbu za kiutumishi vinginevyo watawajibishwa.
Pia alisema wanatambua changamoto zinazowakabili na wanajipanga kushirikiana kwa pamoja kukaa na madereva kuweza kutafuta suluhisho katika usimamiz wa mizani.
“Watumishi na madereva shirikianeni kutokomeza vitendo vya rushwa, kamwe msijihusishe kutoa wala kupokea rushwa kupata huduma za haraka.
“Tukikubaini tutakuchukulia hatua kali za sheria, mambo yote yanayofanyika vituo kama hivi tumeyapata, hivyo badilikeni kabla ya hatua kuchukuliwa,”alisema.
Hata hivyo alitoa wito kwa madereva wa magari ya mizigo wanaotakiwa kuwa na stika maalumu za usafirishaji wa mizigo yao kufuata utaratibu wa kuchukua stika hizo mahali husika kuepusha usumbufu na msongamano wa katika vituo vya mizani.
Akiwa katika eneo la sehemu ya maegesho na kulaza magari mjini Kahama, Kwandikwa, alitoa wito kwa viongozi wa halmashauri hiyo kuchukua hatua kali kwa madereva wanaoegesha nje ya eneo hilo kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Alitoa ushauri kwa uongozi wa halmashauri hiyo kuona namna ya kujenga maegesho mengine kama hayo kupata chanzo cha mapato na kusaidia kuujenga mji kuwa na taswira nzuri.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Shinyanga, Mibala Ndilindi, alisema ni kweli vitendo vya rushwa vinafanyika katika vituo vya mizani.
Alisema tayari hatua za sheria zimechukuliwa kwa watumishi watatu wa mizani ya Mwendakulima.