30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri afanya udalali uuzwaji kiwanda

Dr+marry+nagu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Ubinafsishaji, Dk. Mary Nagu, amehusishwa na kashfa ya udalali katika uuzwaji wa kiwanda cha Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) tawi la Arusha, imebainika.

Dk. Nagu alikuwa Waziri wa wizara hiyo katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu.

Imeelezwa kuwa waziri huyo alikuwa akiandaa mikakati mbalimbali, ikiwamo ya uuzaji wa kiwanda hicho, huku ofisi yake kwa wakati huo ikitumiwa na mfanyabiashara Gullam Dewji katika kukinunua.

Kwa nyakati tofauti, inaelezwa Dk. Nagu alitumia ofisi yake kuratibu vikao kwa kumshirikisha Gullam pamoja na mwekezaji aliyepewa kukiendesha kiwanda hicho, Philemon Mollel ambaye alikodishwa kwa mujibu wa sheria.

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa vita ya kukitaka kiwanda hicho ilianza mwaka 2007 ambapo Serikali baada ya kujiridhisha na taratibu kadhaa, ilikikodisha kwa Kampuni ya Monaban Traning & Faming Co Ltd kupitia Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC).

“Baada ya mwekezaji huyo kupewa kiwanda, kila siku Gullam Dewji alikuwa akienda kwa Waziri Nagu ambaye naye aliwakutanisha zaidi ya mara tatu kwa hoja kuwa washirikiane ili Serikali iwape kiwanda.

“Lakini mara zote Mkurugenzi wa Monaban, Phillemon Mollel, alimgomea Dewji na hata kufikia kuambiwa kama akikataa kuingia naye ubia, atahakikisha hapewi kiwanda licha ya kutimiza masharti yote ya Serikali.

“Hata hivyo, katika vikao vilivyofanyika zaidi ya mara tatu, wakati mmoja Gullam Dewji na Mollel walitaka kushikana na kutwangana ngumi katika ofisi ya Waziri Nagu,” alisema mtoa habari huyo.

 

KAULI YA DK. NAGU

Kutokana na madai hayo, MTANZANIA ilimtafuta Dk. Nagu, ambaye alisema kama kuna jambo lolote alilolifanya, ni vema mwandishi akaenda Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambako anaweza kukuta maagizo aliyoyatoa.

“Mimi siwezi kusemea suala hilo na siku zimekuwa nyingi tangu nilipotoka serikalini, siwezi kukumbuka nini nilichoamua kuhusu kiwanda cha NMC na hata vikao tulivyokaa.

“Ila unaweza kwenda Wizara ya Viwanda ambako ndiko suala la uwekezaji limehamishiwa, huko utapata taarifa zote, sasa muda umepita kidogo, sitaki kusemea hilo,” alisema Dk. Nagu.

 

GULLAM DEWJI

Alipotafutwa Gullam, ambaye ni baba mzazi wa mfanyabiashara mashuhuri nchini, Mohamed Dewji, alisema kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa huku akitaka kuonana na mwandishi.

“Unajua umenipigia, wewe umepata maelezo ya upande mmoja, lakini sasa mimi sitaki kuongea bila kuwa na ‘document’ (nyaraka), hivyo mama anazo na atarejea Ijumaa (leo), njoo Jumamosi (kesho).

“Kama unataka kuandika, ‘I have no problem’ (sina tatizo), mimi sitaki kuzungumza kwa mdomo, nataka kuongea kwa ‘document’, kama yeye (Mollel) anasema kila jambo langu, mimi sitaki kusema,” alisema Gullam.

 

PHILEMON MOLLEL

Akizungumzia suala la kiwanda hicho, Mollel ambaye ndiye Mkurugenzi wa Monaban Traning & Faming Co Ltd, alisema yeye kama mwekezaji mzawa amekuwa akipita katika changamoto kadhaa licha ya kuomba auziwe kiwanda hicho na Serikali.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwapo vita ya kugombea kuuziwa kiwanda kati yake na Ghullam, alisema: “Ni kweli kuna vita kubwa kati yangu na Gullam Dewji, ambaye amekuwa akifanya kila aina ya fitina kunichongea, na hata alifikia kuniambia kama sitaingia ubia naye sitapewa kiwanda hiki na Serikali.

“Ninashangaa ‘mishale’ ninayopigwa na hata kunyanyasika katika nchi yangu, hapa wamekuja viongozi karibu wote wa Serikali kuja kukagua na kusema nimetimiza vigezo vyote. Nimefunga mashine mpya karibu zote na kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 6 ikiwamo pamoja na kulipa wafanyakazi zaidi ya 200 kila mwezi.

“Amekuja Waziri Mkuu mstaafu Pinda, Janeth Mbene, akiwa Waziri mdogo wa Viwanda, Mwingulu (Waziri wa Mifugo, Kilimo na Uvuvi) pamoja na Waziri wa sasa wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na wote hawa wamesifu kazi niliyofanya, sasa sijui kwanini sipewi hiki kiwanda kama wengine walivyobinafsishiwa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles