Na Renatha Kipaka, Kagera
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Dotto Biteko amewasihi wazawa wa Mkoa wa Kagera na walioko nje ya nchi na ndani kukumbuka nyumbani na kurudi kuwekeza ili kuinua uchumi wa mkoa huo.
Ametoa kauli hiyo mapema leo wakati wakati wa tamasha la Ijuka Omuka linaloendelea mkoani Kagera ambalo malengo yake ni kuwahimiza wazawa kurejea nyumbani na kuwekeza katika nyanja mbalimbali.
Hata hivyo amesema kuwa kutokana na Mkoa wa Kagera kupakana na nchi za Afrika ya Mashariki ina fursa kubwa kibiashara.
“Ndugu zangu tamasha hili la Ijuka Omukaya limebeba dhana ya neno la kihaya lenye maana ya kumbuka nyumbani ambalo limeandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa ili kuilejesha Kagera katika nafasi yake, “amesema Dk. Biteko.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Innocent Bashungwa amesema wataendelea kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera ili kuhakikisha wanasukuma mbele maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa amesema Tamasha hili limeleta mafanikio makubwa ikiwa ni kuanzisha viwanda vipya ambavyo vitasababisha kuleta maendeleo chanya kwa vijana.